WASICHANA wawili raia wa Tanzania wamekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakihusishwa na pipi 187 za dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 135 walizokuwa wamezimeza.
Kamanda wa Polisi wa Kikosi Maalumu cha Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa alisema watuhumiwa hao walikamatwa jana saa 11.45 jioni katika uwanja huo.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa na kikosi kazi kinachofanya kazi katika uwanja huo, wakiwa katika harakati za kusafiri na ndege ya Shirika la Qatar kwenda China.
Alimtaja mtuhumiwa wa kwanza kuwa ni Mariam Makuhani (29), mkazi wa Tabata Kimanga aliyekuwa ametoa pipi 65 kwa njia ya haja kubwa.
Mtuhumiwa mwingine ni Hadija Shomari (30), mkazi wa Magomeni Mapipa ambaye alitoa pipi 122 kwa njia ya haja kubwa.
Nzowa alisema kuwa wanaendelea kuwashikilia watuhumiwa hao kwa mahojiano zaidi huku wakiendelea kuzitoa pipi hizo kwa njia hiyo ya haja kubwa.
Alisema wanawake hao walimeza pipi hizo 187 na kila moja ina uzito wa gramu 16. Alisema mara nyingi pipi zenye uzito wa gramu 17 humezwa na wanaume.
-habarileo
No comments:
Post a Comment