Friday, 6 December 2013

WANAODAIWA KUMWUA DK MVUNGI, WATISHANA KUUANA GEREZANI







WASHITAKIWA 10 wanaodaiwa kumwua aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengodo Mvungi wameiomba Mahakama iwatenganishe rumande kwa kuwa wanapigana na kutishana kuuana.
Walidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kesi hiyo ilipotajwa mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo. Washitakiwa hao waliiomba Mahakama iingilie kati suala lao kwa kuwa wakiwa rumande wamekuwa wanatishana kuwa watauana jambo ambalo ni hatari.
Hata hivyo, Hakimu Fimbo aliamua waendelee kukaa huko mahabusu na waelewane na kama jambo lolote litatokea watapewa taarifa na Mkuu wa Gereza.
Washitakiwa hao walidai kuwa hawajuani na wapo gereza moja, lakini wanatishiana kuuana na wameshapeleka malalamiko yao kwa Mkuu wa Gereza lakini hajachukua hatua na kuiomba Serikali ifanye uchunguzi ili ijue aliyefanya mauaji hayo.
“Serikali ikifanya uchunguzi haki itatendeka kabla ya wao kuuana wakiwa mahabusu,” alidai mmoja wa washitakiwa hao huku akionesha majeraha aliyopata mwenzake kutokana na kupigana.
Wakili wa Serikali, Yasinta Peter, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa, Hakimu Fimbo aliamua kesi hiyo itajwe tena Desemba 19.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni Chibago Magozi (32) , John Mayunga (56), Juma Kangungu (29), aliyekuwa mlinzi wa marehemu Dk Mvungi, Longishu Losingo (29), Masunga Makenza (40), Paulo Mdonondo (30), Mianda Mlewa (40), Zacharia Msese (33), Msungwa Matonya (30) na Ahmad Kitabu (30).
Wanadaiwa kuwa Novemba 3 katika eneo la Msakuzi Kiswegere, Kibamba Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, washitakiwa hao kwa pamoja walimwua Dk Mvungi kwa kukusudia.

Source Habari leo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!