Sunday, 8 December 2013
SIMBA KWENDA BUNGENI KUMSHINIKIZA RAGE AJIUZULU
Wanachama wa Simba wanaompinga Mwenyekiti wa klabu hiyo wamethibitisha azma yao ya kwenda Dodoma Jumatano kuonana na Spika wa Bunge Anna Makinda kulalamika namna Ismail Aden Rage anavyovunja katiba yao.
Awali wanachama hao walipanga kuondoka leo kwenda Dodoma ili kesho waonane na spika huyo, lakini wamehairisha kutokana na tarehe hiyo kuwa siku ya Uhuru wa Tanganyika ambapo hakutakuwa na vikao vya Bunge.
Akiongea kwa niaba ya wanachama wenzake Katibu wa tawi la Mzambarauni, Daniel Kamna, mwenye kadi ya uwanachama wa klabu hiyo namba 100, alisema lengo la kwenda Dodoma lipo pale pale licha ya kuingiliwa na siku ya mapumziko kitaifa.
"Juzi (Alhamisi) tulimpa siku mbili awe amejiuzulu... lakini ameonekana kuwa mkaidi na kiburi, Sasa sisi msimamo wetu uko pale pale tumeshajipanga na tumewasiliana na wabunge wanachama wa klabu yetu ambao wametualika bungeni hivyo tutaondoka hapa Jumanne ili siku inayofuata asubuhi tuingine bungeni," alisema Kamna.
Alisema kuwa mwenyekiti wao huyo ameonyesha jeuri na kutowasikiliza wanachama waliomuweka madarakani na badala yake amekuwa na maamuzi ya peke yake yasiyokuwa na faida kwa klabu hiyo.
Kamna alisema moja ya jambo ambalo limewashangaza ni kitendo cha Mwenyekiti huyo kukutana na mmiliki wa klabu ya Sunderland ya Uingereza mapema mwaka huu ambapo badala ya kuomba msaada kwa ajili ya klabu, alipigia debe jimbo lake la Tabora mjini.
"Sasa mtu kama huyo klabuni kwetu wa nini," aliuliza Kamna. "Ameonyesha kuweka maslahi yake binafsi mbele badala ya Simba kwanza."
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment