Wednesday 11 December 2013

DAWA FEKI, MAGARI FEKI, FEDHA FEKI, BIDHAA NYINGI FEKI......

Sasa imefikia hali mbaya ya kibiashara mpaka inatishia amani pamoja na afya za wananchi, mwananchi
hana uhakika wa kupata bidhaa ambayo ipo sokoni ikiuzwa kwa thamani halisi inayolingana na viwango vinavyokubalika. 

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lipo kwa ajili ya kuthibitisha ubora wa bidhaa kwa ajili ya matumizi yanayokusudiwa, lakini bado wafanyabiasara wasio waaminifu wanafanya mbinu za kuwakwepa
 wataalamu hao wa viwango na kuwauzia wananchi  bidhaa zisizokidhi viwango.
 
Tumekuwa tukisikia kwenye redio na runinga pamoja na kusoma matangazo mbalimbali ya kibiashara
 katika magazeti, vyote vikinadi ubora wa bidhaa kwa ajii ya vifaa vya ujenzi, madawa, magari, vyakula
 pamoja na bidhaa nyinginezo, na kwa bahati nzuri bidhaa nyingi zinazoingia katika soko kwa mtindo
 wa kutangazwa zinapitia tathmini ya Shirika la Viwango. 
 
Na kwa bahati mbaya sana bado hatujapata taasisi nyingine zaidi ya TBS ambayo imeidhinishwa
 na serikali kuweka viwango bora vya bidhaa hapa nchini, kama kutajitokeza bidhaa katika masoko
 ya ndani ambazo zitakuwa haziko katika viwango vinavyokubalika, lakini zenye uthibitisho wa kukubalika, basi lawama zitakuwa kwa TBS. 
 
Tumekuwa tukisikia malalamiko kutoka kwa watumiaji wa baadhi ya bidhaa kuwa hazina viwango
 vizuri vya ubora, baadhi ya masoko hapa nchini yamejaa bidhaa zinazolalamikiwa kuwa chini
 ya viwango vya ubora, na bidhaa nyingi kati ya hizo zinafahamika zinakotoka. 
 
Utafiti uliofanywa hivi karibuni unadhihirisha kwa namna hata bei za bidhaa hizo feki zilivyo chini
 kuliko bidhaa za aina ile ile zenye viwango vinavyokubalika. 
 
Wafanyabiashara wakumbuke kuwa kufanya biashara kwa bidhaa zilizo chini ya viwango kuna hatari
 zake, na hatari zenyewe zinatofautiana kutokana na unyeti wa matumizi ya bidhaa kwa walengwa. 
 
Kuuza dawa za matumizi kwa binadamu ambazo hazina viwango ni kuhatarisha maisha ya mlaji, athari
 zake si kama kuuza gari ambalo litadumu kwa muda mfupi kabla halijaanza kukorofisha, athari ya dawa
 zilizo feki kwa matumizi ya binadamu ni ama kuharibu kinga ya mwili au kifo.
 
Hapa nchini sasa kumejaa viwanja vingi vinavyouza magari, magari mengine utaambiwa ni mapya
 wakati magari mengine utaambiwa yametumika kidogo. 
 
Magari mengine utaambiwa yametengenezwa Japan, na ukiyachunguza sana utagundua kuwa yametengenezwa Korea, na ukiwahoji wahusika watakwambia yametokea Korea lakini teknolojia
 yake ni ya Japan. Unabaki kuchanganyikiwa tu, lakini kama mnunuzi alikuwa na nia ya kumumua gari lililotengenezwa Japan, sasa atakuwa anauziwa gari feki kwa maelezo ya kibiashara tu. 
 
Bidhaa nyingi zinaonekana kuwa dhaifu na haziwezi kuhimili matumizi ya muda mrefu, kwa bahati
 mbaya sana hata noti mpya za hivi karibuni zimedhihirika kuwa chini ya viwango, ni noti zinazochakaa
 na kupoteza hadhi yake kwa haraka sana, ni noti ambazo zikipitia mikononi mwa wauza mkaa 
watatu tu unahitaji kuwa mzoefu wa kuzitambua kwa umbile badala ya kuzisoma.
 
Lililo baya zaidi kwa noti kama ya Shilingi elfu kumi, ukipambana na mvua ukanyeshewa na kulowa,
 zenyewe zinatoa rangi, mwishowe sina uhakika kitakachotokea. Ingawa thamani yake haibadiliki
 lakini pia tunaweza kuziita bidhaa feki.
 
Kila kitu kisipokidhi uhalali wa matumizi yake kinabadilika kuwa feki, na hata wakati wa upigaji kura
 wakati wa chaguzi mbalimbali, zipo kura zinazojitokeza bila uhalali, nazo huwa feki kwa vile hazikupitia
 mchakato wa uhalali wake. 
 
Migogoro inayozuka baada ya kugundua kitu kilicho feki ni mikubwa, wengine hudai kupata fidia
 ya gharama walizoingia katika mkataba wa kutumia bidhaa feki bila kujua, lakini lililo kubwa zaid
i sasa ni namna ya kudhibiti biashara ya bidhaa feki nchini.
 
Wakati mwingine athari zinazopatikana kwa kutumia bidhaa feki ni kubwa zaidi, madawa feki ambayo
 yanatumika kwa binadamu madhara yake ni kuathiri mfumo wa uhai wa binadamu, na wakati mwingine kusababisha kifo. 
 
Kutokana na hali halisi ya mfumuko wa maradhi mengi katika kipindi hiki, baadhi ya wataalamu ambao
 wengine huwa feki, wameendelea kutengeneza madawa yaliyo chini ya viwango na ambayo kwa bahati
 mbaya hupenyezwa kinyemela hadi kwa walengwa bila hata kupitia TBS.  
 
Miezi michache iliyopita kulipatikana taarifa kuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA)
 ilikamata aina tano za dawa za bandia mojawapo ikiwa ni dawa ya malaria wakati nyingine ikiwa
 imesambazwa bila ya kusajiliwa kisheria. 
 
Ilifahamika kuwa dawa zilizokamatwa ni aina ya Artemeter+Lumefantrine ambayo ina jina la
 kibiashara 'Coantem' ambayo ni dawa ya mseto inayotibu malaria. 
 
Nyingine ilikuwa dawa ya kutuliza maumivu inayojulikana Ibuprofen inayouzwa kama Erythromycin
 Stearate aina ya vidonge nk.  Mkurugenzi Mkuu wa TFDA Hiiti Sillo alikiri kuwa dawa hizo zilikamatwa
 baada ya kufanyika ukaguzi katika vituo zaidi ya 390 mikoani.
 
Kwa bahati mbaya wasambazaji wa dawa nao hawatoi tahadhari ya aina ya dawa feki kwa wananchi
 labda kwa sababu hata watengenezaji wa dawa hizo nao wanatafuta teknolojia ya dawa halisi 
na kuzifunga katika makasha yanayofanana na dawa zilizoidhinishwa kwa matumizi ya binadamu. 
 
Imefikia hatua mbaya sasa ambapo dawa feki zinatumika kuwarubuni wananchi ambao hawana
 uelewa wa zipi dawa halisi na zipi ni feki, hiyo ni hatari kubwa, na kwa bahati mbaya dawa hizo
 ni za bei poa!
chanzo:Nipashe

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!