Thursday 12 December 2013

BASI LA OSAKA LAPATA AJALI NA KUUA MKOANI KILIMANJARO

Majeruhi wakiwa kwenye gari la wagonjwa kwenye mapokezi ya Hospitali ya Rufani ya KCMC Mkoa wa Kilimanjaro, baada ya kupata ajali ya basi la Osaka kwenye Kijiji cha Kirinjiku, wilayani Same, mkoani Kilimanjaro jana. Picha na Dionis Nyato  


Kilimanjaro na Manyara. 
Watu saba wamefariki dunia na wengine 71 kujeruhiwa kwenye ajali ya iliyohusisha mabasi ya abiria mikoa ya Kilimanjaro na Manyara.

Ajali iliyotokea Mkoa wa Manyara, basi la abiria maarufu Polepole liligongana na trekta na bajaji eneo la Makatanini, Wilaya ya Babati. Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Mussa Marambo alisema ajali hiyo ilitokea Desemba 7, mwaka huu saa 2:00 usiku wakati basi hilo likitokea mkoani Arusha.

Marambo alisema chanzo cha ajali hiyo ni trekta kuegeshwa katikati ya barabara bila alama yoyote ya tahadhari. Basi la abiria aina ya Fusso, mali ya Issack Polepole liligongana na trekta hiyo ambayo haikuwa na namba za usajili aina ya Swaraj, lilikuwa likiendeshwa na Clement Tuji.

Alitaja waliokufa kuwa ni Shaibu Olae (25), Nicodemu Mofuru (27) mkazi wa Majengo Mapya na Mwalimu wa Sekondari ya Aldersgate, Charles Exaud na mwanamke ambaye hakufahamika.

Katika Mkoa wa Kilimanjaro, watu watatu wamefariki dunia papohapo na wengine 39 kujeruhiwa, baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Arusha kwenda Dar es Salaam kupoteza mwelekeo kabla ya kuacha njia na kupinduka.

Ajali hiyo iliyotokea jana saa 3:30 asubuhi eneo la Kirinjiko, Wilaya ya Same, ilihusisha basi la abiria mali ya Kampuni ya Osaka Coach.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

Naye Katibu wa Hospitali ya Wilaya ya Same, Mwajuma Nyika alisema hali za baadhi ya majeruhi wanaopata ni mbaya na kwamba uongozi wa wilaya umetoa magari manne ya dharura kwa ajili ya kuokoa roho za majeruhi wa ajali hiyo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!