Thursday 28 November 2013

TUME YA KATIBA MPYA YAONGEZEWA MUDAWA SIKU 14 ZAIDI KUANZIA DESEMBA 16 MWAKA HUU ILI KUIWEZESHA KUKAMILISHA KAZI YAKE.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameiongezea Tume ya Mabadiliko ya Katiba siku 14 zaidi kuanzia Desemba 16, mwaka huu, 2013, ili kuiwezesha kukamilisha kazi yake. 



Rais Kikwete ameiongeza Tume hiyo muda zaidi kufuatia maombi ya Tume yenyewe na kwa mamlaka aliyonayo chini ya Kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ameongeza muda wa Tume hiyo kufanya kazi kuanzia Desemba 16 hadi Desemba 30, 2013.

Hii ni mara ya pili kwa Rais Kikwete kuiongezea Tume hiyo muda wa kufanya kazi yake. Kufuatia maombi ya kwanza, Rais Kikwete aliiongezea Tume hiyo muda wa siku 45 kuanzia Novemba Mosi hadi Desemba 15, mwaka huu, 2013.

Chini ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Tume hiyo inatakiwa kufanya kazi kwa miezi 18. Aidha, sheria hiyo inampa Rais mamlaka ya kuiongezea Tume hiyo muda wa kufanya kazi usiozidi siku 60.

Kwa uamuzi wake wa kuiongezea Tume hiyo siku nyingine 14, Rais Kikwete atakuwa ameiongezea Tume hiyo muda wa kufanya kazi wa jumla ya siku 59 kati ya 60 ambazo anaruhusiwa kisheria kuiongezea Tume hiyo.

Imetolewa na: 
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu. Dar es Salaam.
27 Novemba, 2013

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!