Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imepiga marufuku biashara
ya kutembeza visu, sime na mapanga barabarani na kusema yeyote
atakayekiuka agizo hilo atakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi
Kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova alisema jeshi hilo lipo katika
mchakato wa kupendekeza sheria mpya ya matumizi ya silaha na umiliki ili
kudhibiti matumizi mabaya yakiwamo uuzaji wa visu, mapanga na sime
kiholela.
Kamishna Kova alisema tatizo kubwa si mtu kumiliki
silaha, bali jinsi watu wanavyozitumia vibaya na kusababisha madhara
katika jamii na kuongeza kuwa sheria hiyo itajumuisha uuzaji holela wa
visu, mapanga na sime barabarani na umiliki wa silaha za moto.
“Kwa mfano visu, kwa kawaida vinatumiwa nyumbani
kukatia nyanya na vitunguu, lakini mtu anaweza kukitumia vibaya kwa
kumchoma nacho mtu tumboni au kifuani...hivyo atakayeonekana anauza vitu
hivyo, atachukuliwa hatua.
Hatua hiyo imekuja baada ya mfululizo wa mauaji ya kutumia silaha za moto yanayohusishwa na wivu wa mapenzi kukithiri nchini.
Novemba 19, mwaka huu, Gabriel Munisi aliwaua watu
wawili kwa risasi na kumjeruhi mpenzi wake, Christina Newa, mama mzazi
wa mpenzi wake, Ellen Eliezer na kisha kujiua, kwa kile kinachoaminika
kuwa ni wivu wa mapenzi.
Mapema Oktoba mwaka huu, Mwandishi wa Habari wa
Kituo cha ITV, Ufoo Saro alijeruhiwa pia kwa risasi na mpenzi wake,
Anthery Mushi. Pia alimuua mama mzazi wa Ufoo na kisha kujiua kwa
kujipiga risasi.
Kamishna Kova alisema pia kuwa katika mchakato huo
wa kuunda sheria mpya za umiliki wa silaha, hatua kali ikiwamo
kunyang’anywa silaha hizo kwa watu wanaozitumia vibaya itachukuliwa.
Hata hivyo, alisema wakati sheria hizo
zikisubiriwa, polisi watawachukulia hatua kali wote watakaobainika
kuzitumia vibaya. Aliwataka Watanzania kuwa makini na matukio ya uhalifu
katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka na sikukuu
No comments:
Post a Comment