Sunday, 10 November 2013

MAZUNGUMZO KUHUSU IRAN YAFIKIA PAZURI

MAZUNGUMZO KUHUSU IRAN YAFIKIA PAZURI


Mazungumzo kati ya Iran na nchi zenye nguvu zaidi duniani yanaingia siku ya tatu huku wanadiplomasia wanaotafuta ufumbuzi wa mzozo kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran wakionya kuwa vikwazo vikubwa bado vipo. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry aliyesitisha ziara yake Mashariki ya kati kuhudhuria mazungumzo hayo kuhusu Iran yanayofanyika mjini Geneva Uswizi, ameonya kuwa bado hakuna maafikiano kwani kuna masuala muhimu sana mezani ambayo bado hayajatatuliwa.
Kerry amejiunga na mawaziri wenzake wa mambo ya nje kutoka Ujerumani,Ufaransa na Uingereza, na matumaini yanaongezeka hasa baada ya taarifa kuwa waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov anatarajiwa kuhudhuria leo.
Kuwasili kwa Lavrov kutawaleta pamoja mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zote wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ambao kwa muongo mmoja wamekuwa wakiujadili mpango wa utatanishi wa kinyuklia wa Iran.Hapo jana, Kerry,mwenzake wa Iran Javad Zarif na mkuu wa sera za kigeni wa umoja wa Ulaya Bi Catherine Ashton anayeziwakilisha nchi sita zenye nguvu zaidi duniani katika mazungumzo hayo walikutana hadi usiku. Mkutano huo uliishia kwa Kerry kusema kuwa bado kuna kazi kubwa inayowakabili kabla ya kuafikiana.Mkutano huo unatarajiwa kuendelea leo asubuhi.
Ikiwa makubaliano yatafikiwa ,basi hatua hiyo itakuwa ya kuuondoa mkwamo ambao umekuweko kwa muongo mzima kati ya Iran na nchi hizo sita zinazojumuisha Ufaransa,Uingereza,Urusi,China,Marekani na Ujerumani.
Makubaliano yanayotarajiwa, yanayozingatiwa kuwa hatua ya kwanza ya kulifikia suluhisho, yatakuwa na maana ya Iran kuzisimamisha shughuli zake za kinyukilia kwa muda wa miezi sita ,ili vikwazo vilivyoubana uchumi wa nchi hiyo vilegezwe.
Ripoti zinaarifu kuwa makubaliano yanayopendekezwa huenda yakawa na maana ya Iran kuacha kuyarutubisha madini ya urania kwa asilimia 20.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!