Na Anna Nkinda – Maelezo
Serikali
ya Japani kupitia Ubalozi wake nchini imetia saini mkataba na shule ya
Sekondari ya wasichana ya WAMA-Nakayama iliyopo Rufiki mkoani Pwani kwa
ajili ya msaada wa vifaa vya maabara, ujenzi wa zahanati na kutoa
mtambo wa maji wa kutumia genereta utakaogharibu Shilingi milioni mia
moja na sabini.
Utiwaji
saini wa makubaliano hayo ulifanyika jana katika shule hiyo ambayo ni
ya watoto yatima, maskini na wanaoishi katika mazingira magumu kati ya
balozi wa Japani Nchini Masaki Odaka na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete
ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) na
kushuhudiwa na wageni mbalimbali akiwemo Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete
aliyekuwa katika ziara ya kikazi wilayani Rufiji.
Akiongea
mara baada ya utiwaji saini wa makubaliano hayo Rais Dk. Kikwete
aliwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii kwani wametoka katika mazingira
magumu, maskini na wengine ni yatima elimu peke yake ndiyo
itakayowakomboa kimaisha na kuwapeleka katika mazingira mazuri.
Rais
Dk. Kikwete pia alimpongeza Mke wake Mama Salma Kikwete kwa kufikiria
kuwa na wazo la kuanzisha shule kama hiyo ambayo leo hii imewapa
nafasi ya kusoma katika mazingira mazuri watoto wa kike
wanaotoka katika mazingira magumu na kuwataka kutumia nafasi
hiyo kusoma kwa bidii kwani walimu walio nao ni wazuri na mazingira ya
shule ni mazuri.
“Sisi
wazee wenu tupo, tutaendelea kuwasaidia na kuwaunga mkono ili mpate
mafanikio, hakuna kingine tutakachoweza kuwaombea zaidi ya hili, mmetoka
katika mazingira magumu wengine ni yatima elimu ndio itakayowatoa
katika mazingira hayo na kuwafikisha katika mazingira mazuri,” alisema
Rais Dk. Kikwete.
Rais
Dk. Kikwete pia aliwapongeza wanafunzi hao kwa kufanya vizuri katika
mitihani yao ya kidato cha pili na kushika nafasi ya kwanza kiwilaya na
kuwataka kufanya vizuri zaidi ili waweze kuongoza hadi ngazi
ya taifa.
Kwa
upande wake Balozi Odaka alisema wazo la mradi huo wa kuboresha
mazingira ya kusomea kwa wanafunzi ulianza miaka kadhaa iliyopita baada
ya uzinduzi wa shule hiyo na Taasisi ya Nakayama ya nchini Japani.
Alisema
mradi huo unasura tatu ambazo ni kutoa vifaa vya maabara, kutayarisha
zahanati yenye vifaa na kutoa mtambo wa maji ya kutumia genereta karibu
na zahanati na mabweni. Msaada huo utaboresha mazingira ya kusomea kwa
wanafunzi, kufanya kazi kwa wafanyakazi wote wa shule hiyo pamoja na
shule jirani ya Sekondari ya Nyamisati.
“Pamoja
na mradi huu kama kuna mahitaji mengine zaidi ya kuboresha mazingira ya
kusomea shuleni hapa, Serikali ya Japani ingependa kuzingatia ili
kuridhisha mahitaji ya wanafunzi kwani tunapenda kuendeleza misaada ya
mahitaji muhimu ya kibinadamu nchini Tanzania”, alisema Balozi Odaka.
Aidha
Balozi huyo pia alimpongeza mama Kikwete kwa mchango wake wa maendeleo
ya wanawake nchini na kusema kuwa shule hiyo na mradi huo usingekuwepo
bila ya jitihada zake.
Naye
Mama Kikwete aliwashukuru watu wa Japani kwa msaada muhimu wa maendeleo
ya kitaaluma utakaosaidia kuboresha ufundishaji wa majaribio ya masomo
ya sayansi na huduma ya afya kwa wanafunzi na Jumuiya ya WAMA-Nakayama .
Mwenyekiti
huyo wa WAMA alisema lengo kuu la shule hiyo ni kutoa elimu bora ya
Sekondari kwa watoto wa kike waliotoka katika mazingira hatarishi na
yatima kwani elimu ni nyenzo muhimu ya kumuwezesha mtu kujikwamua kutoka
katika hali ya umaskini, ujinga na maradhi.
“Elimu
ya Sekondari kwa mtoto wa kike inamuwezesha kuepuka mimba za utotoni ,
vifo vinavyotokana na uzazi kwani asilimia 20 ya vifo vya kina mama
vinatokana na uzazi katika umri mdogo. Pia elimu itawasaidia kufaidika
na fursa mbalimbali za elimu ya juu na kujiendeleza kiuchumi”, alisema
Mama Kikwete.
Alisema
wamejenga maabara nne ambazo zitawezesha ufundishaji wa masomo ya
sayansi na kupatikana kwa vifaa hivyo kutawasaidia wanafunzi kutekeleza
mafunzo kwa vitendo kwa kiwango cha juu na hivyo kuongeza ufaulu katika
mitihani yao.
Akisoma
taarifa ya shule Kaimu Mkuu wa Shule Mwalimu Suma Mensah alisema shule
hiyo ni kipekee kwani inachukua wanafunzi kutoka Tanzania nzima ambao
wanatoka familia duni, mazingira magumu na yatima.Shule inawasaidia
kwa asilimia mia moja kwa kuwapatia chakula,malazi na mavazi,
kuwapatia nauli wanaporudi nyumbani wakati wa likizo na wanaporudi
shule na pesa kidogo za matumizi wanapokuwa safarini.
Mwalimu Mensah
alisema wamekuwa na mikakati kadhaa ya kuboresha taaluma ikiwa ni
pamoja na kuongeza muda wa ziada wa kufundisha na kuwasaidia wanafunzi.
Lengo kubwa ni kumaliza sillabasi mapema na kuanza kufanya marudio ili
wanafunzi waweze kuelewa zaidi na kuandaa mitihani mingi ya ndani na nje
ya shule hii ikiwa ni maandalizi ya mitihani mbalimbali ya kitaifa.
“Tunamshukuru
Mama yetu mpendwa Salma Kikwete kwa kutuletea Mtaalamu wa kompyuta ili
aweze kutufundisha.Tunaamini baada ya kumalizika kwa kozi hii,walimu
tutakuwa na uwezo wa kuandaa masomo yetu kwa kutumia kompyuta na
kufundisha kwa njia ya kisasa yaani ‘projector’ madarasani”, alisema.
Shule
ya WAMA-Nakayama iko chini ya Taasisi ya WAMA ilianzishwa mwaka 2010
ikiwa na wanafunzi 82, walimu watano na wafanyakazi wasio walimu watano
ilizinduliwa mwaka 2011.Hivi sasa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 322
wa kidato cha kwanza mpaka cha nne na wafanyakazi ishirini na saba
27,walimu16 na wafanyakazi wasio walimu 11
No comments:
Post a Comment