Saturday, 12 October 2013

MFANYABIASHARA MWINGINE ALIYEHUSIKA NA MAUAJI YA BILIONEA MSUYA AKAMATWA..

 

Robert Boaz(3)-2Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz
Wakati sakata la mauaji ya bilionea wa madini ya Tanzanite, marehemu Erasto Msuya (43), aliyeuawa kwa kupigwa risasi Agosti 13, mwaka huu, likiwa ‘bichi’ kutokana na kuvuta hisia za wakazi wa miji ya Arusha na Moshi, Polisi mkoani Kilimanjaro wamemtia nguvuni mtuhumiwa muhimu katika kesi hiyo.
Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linasema kuwa mtuhumiwa huyo ambaye kwa sasa jina lake limehifadhiwa, alikamatwa mkoani Kigoma baada ya kusakwa kwa muda mrefu.
Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, mkazi wa Babati, mkoani Manyara, kunafanya idadi ya waliokamatwa hadi sasa kufikia wanane. Tayari saba wameshafunguliwa mashtaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa Kilimanjaro kwa shtaka la mauaji ya kukusudia.
Miongoni mwa waliokamatwa na kufunguliwa mashtaka wamo wafanyabiashara na wachimbaji wadogo wa madini ya tanzanite yanayopatikana katika eneo la Mererani, Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara.Ksoma zaidi bofya
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, aliliambia NIPASHE kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa wiki iliyopita mkoani Kigoma.
Alisema hivi sasa anashikiliwa na kuhojiwa na makachaero wa Jeshi la Polisi kabla ya kuunganishwa na wenzake katika kesi inayowakabili ya mauaji ya kukusudia.
“Huyu (anamtaja), alikamatwa wiki iliyopita huko Kigoma na kwa sasa tunamshikilia na kumhoji ili upepelezi utakapokamilika aunganishwe na wenzake katika kesi ya msingi inayowakabili,” alisema Kamanda Boaz.
Mbali na mtuhumiwa huyo, wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Sharif Mohamed Athuman (31), ambaye ni mchimbaji mdogo wa madini na mkazi wa Kimandolu, mkoani Arusha, Shaibu Jumanne Saidi maarufu kama ‘Mredi’ (38), mkazi wa Songambele, Wilaya ya Simanjiro na Mussa Juma Mangu (30), mkazi wa Shangarai Kwa Mrefu, mkoani Arusha.
Wengine ni Joseph Damas Mwakipesile maarufu kama ‘Chusa’ (36), mfanyabiashara wa madini na mkazi wa Arusha, Jalila Zuberi Said (28), mkazi wa Babati, Sadiki Mohammed Jabir maarufu kama Msudani ama Mnubi (32), mkazi wa Dar es Salaam na Lang’ata, wilayani Hai na Karim Kihundwa (33), mkazi wa kijiji cha Lawate, Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.
Kesi hiyo ya mauaji ya bilionea wa tanzanite, aliyeuawa Agosti 7, mwaka huu, saa 6:30 mchana kwa kupigwa risasi kando kando ya barabara kuu ya Arusha-Moshi, eneo la Mijohoroni, Wilaya ya Hai, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) na kufariki dunia papo hapo, imekuwa ikivuta hisia za wakazi wa mikoa ya Kaskazini kutokana na uwezo wa kiuchumi aliokuwa nao Msuya kabla ya kifo chake.
Mbali na migodi aliyokuwa akiimiliki, marehemu Msuya alikuwa akimiliki pia vitega uchumi vingine kama hoteli ya kifahari ya nyota tano ijulikanayo kama SG Resort iliyopo Sakina jijini Arusha.
Msuya alifika eneo hilo akiwa peke yake baada ya kupigiwa simu na watu anaowafahamu kwenda kufanya nao biashara inayohisiwa kuwa ni ya madini ya tanzanite.
Chanzo: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!