Ili kuimarisha biashara, Ubalozi wa
Uingereza nchini umesema, kuanzia sasa Watanzania wanaotaka huduma za viza kwa
ajili ya kwenda nchini humo wanaweza kupata huduma hiyo katika kipindi cha muda
mfupi kutokana na kuanzishwa kwa kile kinachoitwa ‘viza za
kipaumbele’.
Huduma hiyo ambayo pia imeanza kutumika
katika nchi nyingine za Uganda na Kenya inaelezwa kuwa ni moja ya mkakati wa
Serikali ya Uingereza kuongeza kasi ya ushirikiano na uwekezaji
nchini.
Balozi wa Uingereza nchini, Dianna Melrose
alisema uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizi mbili umeimarika zaidi katika
miaka ya hivi karibuni hivyo kuanzishwa kwa huduma hiyo mpya kutasaidia
kuharakisha kufikia malengo ya kibiashara kwa pande zote.
“Huduma hii ya kipaumbele itahakikisha
maombi ya viza yanafanyiwa kazi ndani ya siku tano na mwombaji atatakiwa kulipia
kiasi cha Sh250,000,” alisema Balozi Melrose.
Hata hivyo, alifafanua kuwa, pamoja na
kuanzishwa kwa huduma hiyo mpya, zoezi la utoaji viza litaendelea kufanywa kwa
kufuata sheria za kawaida za uhamiaji.
Viza hizo za kipaumbele zinatazamiwa
kutolewa katika makundi mbalimbali ikiwamo wafanyabiashara, wanafunzi na wale
wanaokwenda kwa matembezi ya kawaida.
Alisisitiza kuwa viza za kipaumbele zina
lengo la kufanya mchakato wa maombi kuwa wa kasi zaidi hasa kwa wafanyabiashara
pamoja na wengine ambao watahitaji kufanya maombi ndani ya muda
mfupi.
“Tunafanya hivi kutokana na maombi ya
wengi, pia kutokana na kukua kwa uhusiano wa kibiashara ili kuleta maendeleo na
ajira kwa Watanzania na Waingereza,” alisema Balozi
Melrose.
Kuhusu utoaji viza kupitia ubalozi wake
Nairobi, Kenya, Balozi Melrose alisema “Tunafanya hivyo ili kuwa na ufanisi
mzuri wa kazi na hakuna upendeleo wowote.”
No comments:
Post a Comment