SERIKALI ya Tanzania na Uswisi zimetiliana mkataba makubaliano wa kuisaidia mpango wa taifa wa kupambana na malaria nchini (NMCP) nchini wenye thamani ya Sh. bilioni 10.3.
Mkataba huo wa makubaliano hayo umetiwa saini leo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi Dkt. Servancius Likwalile na Balozi wa Uswisi nchini Olivier Chave.
“Nimefurahi kubainisha kuwa lengo kuu la kutia saini makubaliano ya msaada huu ni kupunguza vifo vya watoto na akinamama vinavyosababishwa na ugonjwa wa malaria hasa makundi hayo hatarishi kwa kuimarisha na kusaidia NMCP,” alisema Dkt. Likwalile.
Dkt. Likwalile alisema kuwa Serikali ya Tanzania inaichukulia Serikali ya Uswisi kuwa ni moja kati ya rafiki waaminifu katika masuala ya maendeleo.
Alisema kwa takwimu za hivi karibuni, matokeo yanaonesha kuwa kumekuwa na maboresho mazuri hasa katika kuzuia malaria kwa watoto chini ya umri wa miezi sita hadi 59 vimepungua zaidi ya nusu kutoka asilimia 18 mwaka 2007 hadi asilimia 10 mwaka 2012.
Aidha Dkt. Likwalile alisema kuwa kumekuwa na maendeleo mazuri ya kupambana na ugonjwa wa malaria licha ya changamoto mbalimbali zinazoikumba sekta ya afya.
Changamoto hizo ni pamoja na ukweli kwamba kwa upande wa Tanzania Bara, ugonjwa wa malaria bado ni tatizo kubwa linalowasumbaua Watanzania walio wengi ambapo zaidi ya asilimia 93 bado wanaishi katika mazingira hatarishi ya uwezekanao wa kuambukizwa ugonjwa huo.
Aliongeza kuwa madhara yanayotokana na ugonjwa huo yanaiathiri jamii katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu ambapo wanafunzi hushindwa kumudu masomo hasa wanapokuwa.wagonjwa.
Pia wafanyakazi na wakulima wanapougua hushindwa kutekeleza majukumu yao . Hivyo kupelekea familia na jamii kushindwa kuendesha maisha yao ya kila siku.
Kwa upande wake Balozi wa Chave alisema kuwa matokeo yanaonesha Tanzania inafanya vizuri katika kupunguza ugonjwa wa malaria ambapo takribani asilimia 91 ya wakazi wanatumia vyandarua, asilimia 72 ya watoto chini ya miaka mitano na asilimia 74 ya wanawake wajawazito hulala katika vyandarua vilivyowekwa dawa ya kuzuia mbu.
“Lengo la mradi ni kusaidia NMCP katika kuzuia kuudhibiti na kutibu ugonjwa wa malaria hasa katika kusimamia, kupima na kutoa dawa za malaria kwa ufanisi mkubwa,” alisema Chave.
Balozi Chave alisema kuwa mradi huo unaofadhiliwa na nchi yake umekuwa na mafanikio makubwa ambapo takribani asilimia 48 ya vifo vya watoto wa umri wa chini ya miaka mitano vimepungua kati ya mwaka 2000 hadi 2010.
Kwa mantiki hiyo Balozi Chave alisema kuwa Tanzania inaweza kufikia malengo ya millennia namba nne ifikapo 2015 ambapo ni nchi chache za Afrika zinaweza kufikia malengo hayo.
Naye Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Donan Mmbando alithibitisha kuwa wizara yake itasimamia fedha hizo kulingana na malengo yaliyokusudiwa.
Ushirikiano huo wa maendeleo baina ya nchi hizo ulianza kati ya miaka ya 1960 uliolenga katika kudhibiti malaria wilaya ya Ifakara mkoa wa Morogoro na mwaka 1981 serikali hiyo kupitia Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC) lilijikita katika utoaji huduma za afya kwa lengo la kuendeleza upatikanaji wa huduma bora za kiafya maeneo ya vijijini.
No comments:
Post a Comment