Ni dhahiri kwamba wanaume watashtuka, lakini huenda nao wakashiriki uzazi wa mpango bila upasuaji
Vidonge vya uzazi wa mpango vimezoeleka kutumiwa zaidi na wanawake pekee, kiasi kwamba ni jambo la ajabu kusikia kuwa wanaume nao wanaweza kuvimeza.
Hata hivyo, watafiti mbalimbali wamefanikiwa kutengeneza vidonge vya uzazi ambavyo vinazifanya mbegu za kiume katika mfuko wa uzazi wa mwanamume zisiwe na nguvu ya kuweza kutungisha mimba. Utafiti wa dawa hiyo ambao umewaumiza kichwa wanasayansi kwa miaka mingi umewezesha kupatikana kwa vidonge hivyo ambavyo havina vichocheo kama vile wanavyotumia wanawake ambavyo huingia katika mfuko wa mbegu za uzazi na kisha kuzidhoofisha.
Matokeo ya utafiti huo ambayo yalichapishwa Agosti mwaka huu yanaonyesha kuwa vidonge hivyo vya uzazi kwa wanaume vitazuia kutunga mimba bila ya kuathiri uwezo wa mwanamume kushiriki tendo la ndoa kama kawaida.
Dk James Brander wa Taasisi ya Dana-Farberanasema utengenezaji wa vidonge vya uzazi wa mpango kwa wanaume umekuwa na changamoto kubwa kutokana na upatikanaji wa dawa ambazo zinaweza kuzuia mfumo wa utengenezwaji wa seli za mbegu za kiume.
Vidonge hivyo vilichanganywa na vichocheo vya ‘Desogetrel’ ambazo huzuia uzalishwaji wa mbegu za kiume.
Profesa Malise Kaisi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Shirikishi Muhimbili (Muhas) ambaye ni Mtanzania wa kwanza kuzalisha watoto kwa njia ya upandikizaji (IVF) anasema ana wasiwasi mkubwa kuhusu dawa hizo kutumiwa kwa wanaume.
“Dawa za uzazi wa mpango ni rahisi kutumiwa na wanawake kwa sababu wanawake wana mfumo mwepesi kwa dawa kufanya kazi na kuzuia utungishwaji wa mimba,” anasema.
Hata hivyo, Profesa Kaisi anahisi kwa wanaume itakuwa hatari kwao kutumia dawa hizo kwani kunaweza kusababisha hata kuua kabisa uzalishwaji wa mbegu.
“Wanaume wana maumbile tofauti na mwanamke. Korodani za mwanaume ni kama kiwanda kinachofanya kazi usiku na mchana. Kwa siku moja mwanamume anazalisha mbegu milioni 10,” anafafanua Prof. Kaisi.
Katika kuzifanyia utafiti, panya dume alipewa dawa hizo, kisha akawekwa pamoja na mwenza wake ambapo licha ya kujamiiana hata baada ya miezi kadhaa panya jike hakupata mimba
Utafiti huo ulibaini kuwa pamoja na kuzuia uzalishwaji wa mbegu, vilevile dawa hizo zilionekana kuwa hazina madhara yeyote kwa kuwa hazina mchanganyiko wa vichocheo vya aina yoyote.
“Hazikuwa na madhara ya vichochezi (hormone). Mwanamume atakayezitumia hatabadilika tabia au mwili kupata mabadiliko yeyote yale” anasema Dk Martin Matzuk, mtafiti mwingine wa dawa hizo.
Dk Matzuk anasema hakuna kinga yeyote nyepesi ya uzazi wa mpango kwa wanaume iliyowahi kugunduliwa tangu kugunduliwa kwa mipira ya kiume miongo kadhaa iliyopita.
Inaelezwa kuwa utafiti huo ni mkubwa na utakaoleta mapinduzi katika uzazi wa mpango baada ya vidonge vya uzazi kwa wanawake kuonekana na upungufu kadhaa.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Cyriel Massawe wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Shirikishi Muhimbili , anasema iwapo kweli dawa za uzazi wa mpango zitagunduliwa basizitasaidia wanandoa kujadili namna bora zaidi ya kupanga uzazi.
“Wenza wanapokuwa na uchaguzi wa kutosha wa namna ya kupanga uzazi inawasaidia wote wawili. Kwa mfano kama mama ana matatizo kadhaa, basi baba atachukua jukumu la kutumia vidonge ili kupanga uzazi,” anasema Dk Massawe.
Anasema kwa sasa wanaume wana njia moja tu ya kupanga uzazi ambayo ni mipira ya kiume hivyo basi iwapo njia nyingine zaidi zimepatikana basi itasaidia.
Dk Massawe anasema vidonge vya uzazi wa mpango kwa wanaume bado vina changamoto kwa sababu ya mfumo wa uzazi wa mwanamume.
“Zile dawa zinatakiwa zikazuie uzalishwaji wa mbegu kwa wanaume kwa hiyo ili kuingilia mfumo wa uzalishwaji na pindi mwanamume atakapoacha kutumia awe kama kawaida…ni changamoto” anasema.
Hata hivyo, Dk Massawe anasisitiza kuhusu ushirikiano wa wenza katika kupanga uzazi na kusema kuwa, ni suala linalohitaji watu wawili kujadiliana ili kujua ni njia ipi na salama ya uzazi wa mpango.
Anaongeza kuwa wenza wanapopanga uzazi itawasaidia kuimarisha afya zao, za watoto na hata kupunguza mzigo wa majukumu ambayo hayakutarajiwa.
Utafiti mwingine unaofanana na huu ulifanywa mwaka 2010 ambapo wanasayansi waliwauliza wanawake na wanaume iwapo wanaume wanaweza kutumia dawa za uzazi wa mpango pindi zitakaposhauriwa na
Katika utafiti huo ulioongozwa na Dk Judith Eberhardt wa Chuo Kikuu cha Masuala ya Jamii,wanaume, 140 na wanawake 240 waliulizwa kuhusu matumizi ya vidonge vya uzazi wa mpango kwa wanaume.
Hata hivyo matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa ingawa wanaume wote walisema watafurahi kutumia vidonge hivyo lakini wanawake walipata hofu iwapo wenza wao watakubali kutumia vidonge hivyo au kuvitumia inavyotakiwa ili kuimarisha uzazi wa mpango.
Katika utafiti huo, wanaume walio kwenye mahusiano ya kudumu walitoa maoni ya kuvikubali vidonge hivyo huku wale walio katika mahusiano ya muda mfupi waliikosoa njia hiyo ya uzazi wa mpango.
Mei 2009, wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Manchester, Uingereza walitumia wanawake na wanaume kuzifanyia utafiti njia za uzazi wa mpango kwa wanaume kujua iwapo zinafanya kazi ipasavyo na zina manufaa.
Watafiti hao waliwaambia wenza walioshiriki katika utafiti huo kuwa wanaume pekee watumie njia za uzazi wa mpango huku wanawake wakiambiwa kutotumia njia yeyote ili kupima iwapo njia za uzazi wa mpango zinafanya kazi kwa ubora au la.
Hata hivyo, wanaume kadhaa nchini walioulizwa iwapo watakubali kutumia njia yeyote ya uzazi wa mpango ikiwemo vidonge na wanaume wanane kati ya kumi, walikataa kutumia njia yeyote ile.
Mmoja wao, Edwin Mnzeru anasema, yeye na mke wake hawawezi kutumia njia ya uzazi wa mpango ya vidonge, mipira ya kiume, wala ya kitanzi kwa sababu zina madhara kiafya na ni kinyume na dini.
chanzo:mwananchi
No comments:
Post a Comment