Kiwanda bubu cha kutengeneza silaha za aina mbalimbali
ikiwemo bunduki aina ya gobore na bastola, kimebainika kuwepo kati kati ya mji
wa Morogoro, katika eneo la kwa Mavumila.
Eneo hilo ni maarufu kwa utengenezaji wa funguo, ambapo
watu kadhaa wamekamatwa na wanahojiwa na polisi kutokana na tukio
hilo.
Waandishi wa habari waliofika eneo la tukio,
walishuhudia ulinzi mkali ukiwa umeimarishwa eneo la Masika, mtaa wa Kingo,
kwenye nyumba ya marehemu Mavumila, ambayo imekuwa maarufu kutokana na
matengenezo ya funguo.
Polisi kwa kushirikiana na kikosi cha kuzuia ujangili,
idara ya wanyamapori, wamegundua kiwanda bubu cha kutengeneza silaha, na kukuta
mitambo, malighafi na silaha zilizokamilika ikiwemo bunduki kadhaa
zilizokamilika na ambazo zilikuwa bado katika matengenezo, kwenye nyumba
hiyo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kingo, Mwajuma Ndege, aliyekutwa
eneo la tukio, alieleza kushangazwa na hali hiyo, ingawa alikiri miaka ya nyuma
eneo hilo lilitumika kwa matengenezo ya funguo, sambamba na kusafisha
magobore.
Ndege alisema suala la kuwepo kwa kiwanda hicho bubu
huku majirani wakiwa hawafahamu, ni hatari kwa hali ya kiusalama, na kwamba hata
yeye kama kiongozi wa mtaa, hakudhani kama kuna kiwanda kilichosheheni mitambo
na malighafi za hatari namna hiyo.
Naye Ernest Mhando, mkazi wa Morogoro, alisema kiwanda
hicho ni cha muda mrefu, na kimekuwa kikitumiwa kwa matengenezo ya funguo hivyo,
lakini ili kuhakikisha usalama wa watanzania ni vyema wanaohusika na usajili wa
viwanda wakaweka wazi iwapo kina uhalali wa kutengeneza
silaha.
Watuhumiwa kadhaa wameweza kutiwa mbaroni katika tukio
hilo, ingawa kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile, aliahidi
kukutana na waandishi wa habari siku ya Jumapili, kwaajili ya kutolea ufafanuzi
kuhusiana na kiwanda hicho bubu cha silaha.
SOURCE::NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment