Chama cha Wasafirishaji wa Mafuta Tanzania (Tatoa), kimesema Rwanda na Uganda zitajitoa kutumia Bandari ya Dar es Salaam kuanzia Septemba Mosi, mwaka huu.
Katibu Mtendaji wa Tatoa, Zacharia Hanspope aliwaambia waandishi wa habari jana baada ya kukutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuwa nchi hizo zinajitoa kutokana na matatizo mbalimbali ambayo kwa muda mrefu zimekuwa zikiyalalamikia lakini Serikali haikuchukua hatua.
Hanspope alisema ushuru wa barabara na ushuru wa forodha ni baadhi ya vikwazo ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa kwa muda mrefu na wafanyabiashara mbalimbali wa nchi hizo.
“Serikali ipunguze gharama za ushuru wa barabara na ushuru wa forodha ili kuwa na ushindani sawa na bandari nyingine na hivyo kuzivutia kutumia Bandari ya Dar es Salaam,” alisema Hanspope.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Omary Chambo alikataa kuzungumzia lolote kuhusu suala hilo akisema halina mantiki yoyote kwake.... “Hivi hilo jambo unaloniuliza lina sense (mantiki) yoyote? Mie siwezi kujibu lolote nenda ukamuulize mwenyewe (Hanspope) maana wakati akisema mimi sikuwepo.”
Alisema kujitoa kwa Rwanda na Uganda kuitumia Bandari ya Dar es Salaam hakutakiathiri chama hicho tu, bali uchumi wa taifa kwa ujumla.
Hayo yanatokea wakati Rwanda ikiendeleza vita yake ya maneno na Tanzania na mfululizo wa matukio ya kuitenga Tanzania kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki. Viongozi wa Kenya, Rwanda na Uganda walikutana Juni 25, mwaka huu mjini Entebbe, Uganda na kukubaliana kuongeza uhusiano wa kibiashara baina yao.
Kamati ya Bajeti:
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge alisema katika kikao kijacho cha Bunge, kamati hiyo itaibana Serikali kuhusu mikakati inayofanywa kukabiliana na ushindani wa kibiashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema sababu ya Rwanda na Uganda kujitoa kutumia Bandari ya Dar es Salaam ni vikwazo katika barabara ikiwamo mizani mingi ya kupimia mizigo.
“Mizani ni mingi pia kuna usumbufu katika kupima mizigo yao na kwamba hali hiyo inawaletea usumbufu wafanyabiashara wengi,” alisema.
Alisema vitendo vya askari wa usalama barabarani kudai rushwa pia ni miongoni mwa vikwazo pamoja na urasimu mkubwa katika utoaji wa mizigo bandarini ikilinganishwa na bandari nyingine.
“Ni lazima tujifunze kwa majirani zetu Msumbiji, upanuzi wa haraka wa Bandari ya Beira umekuwa kikwazo kwetu, kampuni nyingi zimeanza kuitumia bandari hiyo,” alisema.
Chenge alikitaka chama hicho kuiandikia kamati hiyo mapendekezo yake ikiwa ni hatua ya kunusuru uchumi wa nchi ili waweze kuijadili bungeni.
Umoja wa nchi tatu:
Marais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Paul Kagame wa Rwanda na mwenyeji wao Yoweri Museveni walikutana mjini Kampala, Uganda na kuamua kuitumia Bandari ya Mombasa kwa shughuli zao.
Waliahidi kuimarisha ufanisi katika huduma za Bandari ya Mombasa ili kuhakikisha bidhaa zinafika mapema Uganda na Rwanda.
Pia walikubaliana kujenga reli mpya ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka Mombasa kwenda Kenya na Uganda.
Viongozi hao walikubaliana pia kushirikiana katika sekta ya nishati hasa ikizingatiwa kuwa Uganda imegundua mafuta.
Nchi hizo tatu ambazo zimeruhusu kwa raia wao kusafiri kwa vitambulisho pale wanapotembelea nchi tatu miongoni mwao, zitakutana tena Kenya mwezi huu.
Source:Mwananchi
No comments:
Post a Comment