MWANAMUME mmoja amemnyonga hadi kufa mke wake na yeye akauawa na wananchi wenye hasira, katika Wilaya ya Bunda mkoani Mara. Tukio hilo lililothibitishwa na polisi wilayani hapa, lilitokea usiku wa kuamkia juzi katika Kijiji cha Kisangwa Kata ya Mcharo, kwenye sherehe ya ufunguzi wa nyumba ya ndugu yao.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mcharo, Waziri Kingi, alimtaja mwanamke aliyeuawa kwa kunyongwa na mume wake kuwa ni Paulina Samson Misinzo. Kingi alimtaja mwanamume huyo ambaye pia aliuawa na wananchi wenye hasira, baada ya kukimbilia mlimani kuwa ni Batule Masanja, mkazi wa kijiji hicho.
Imeelezwa kuwa siku ya tukio mwanamume huyo aliyekuwa amekwishatengana na mke wake kwa zaidi ya miezi miwili baada ya kutokea ugomvi wa kifamilia, alimfuata mke wake kwenye sherehe hiyo usiku.
Imedaiwa kuwa baada ya kufika nyumbani hapo huku akiwa na watoto wao wawili, alimuita mke wake aliyekuwa anacheza muziki na kumpeleka nyuma ya nyumba, ambapo alimnyonga kwa kutumia mikono yake hadi kufa.
Taarifa hizo zilieleza kuwa baada ya kumaliza unyama huo, mwanamume huyo alibeba mwili wa marehemu mkewe na kuutupa pembezoni mwa nyumba ya jirani.
“Alifika na watoto wao wawili na baada ya kufika alimuita na kumtoa pembeni….sasa sisi tukadhani kuwa labda anaongea naye tu huko nyuma, kumbe huko ndiko alikomnyongea,” alisema mwanafamilia mmoja.
Mashuhuda walisema kuwa baadaye mwanamume huyo alikimbilia mlimani na kwamba, wananchi wenye hasira kesho yake asubuhi walipiga yowe na kuanza kumsaka na baada ya kumpata walimshushia kipigo kikali kilichoondoa uhai wake.
Walisema kuwa mwanamume huyo aliachana na mke wake, kutokana na kumpiga kila siku alipokuwa akirejea nyumbani akiwa amelewa na ndipo mwanamke huyo alipoamua kwenda kwao.
MPEKUZI.
No comments:
Post a Comment