Wanajeshi wanne wa kutunza amani wa Umoja katika eneo la Darfur nchini Sudan hawajulikani waliko baada ya kusombwa na mafuriko.
Afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa, Rania
AbdulRahman, amesema kuwa wanajshi hao walikuwa wakisindikiza msafara wa
magari ya kutoa misaada, wakati waliposombwa na maji.
Afisa huyo amesema kuwa wanajeshi wengine wawili walipatikana wakiwa hai na kundi la uokoaji.
Shirika la Umoja wa Mataifa wa Afya Duniani WHO,
limesema kuwa zaidi ya watu laki tatu nchini Sudan, wameathiriwa na
mafuriko na zaidi ya watu hamsini wamefariki mwezi huu.
Shirika hilo limesema kuwa eneo linalokaribia
mji mkuu wa Khartoum ndilo limeathirika zaidi na mafuriko hayo ambayo
ndiyo mabaya zaidi kuwahi kukumba eneo hilo kwa zaidi ya miaka ishirini
na mitano iliyopita.
Kikosi cha Umoja wa Mataifa na kile cha Muungano
wa Afrika katika eneo hilo la Darfur, UNAMID, ndilo kubwa zaidi duniani
na lina zaidi ya wanajeshi elfu ishirini.
Wanajeshi hao wa kutunza amani walikuwa
wakielekea eneo la Misterei, takriban kilomita hamsini, Kusini Magharibi
mwa mji mkuu wa eneo hilo Geneina, na msafara wa shirika la Umoja wa
Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP, wakati msafara wao uliposomba
na mafuriko.
Msemaji wa WFP Amor Almagro amethibitisha kuwa
wafanyakazi wa shirika hilo la WFP waliokuwa kwenye msafara huo, watano
kati yao raia wa Sudan na wawili wa mataifa ya Kigeni wako salama.
Umoja wa Mataifa haujatoa majina au uraia wa wanajeshi hao ambao hawajulikani waliko.
Mwaka uliopita, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa
Ban Ki-moon, alilieleza baraza la usalama la Umoja huo kuwa wanajeshi
watatu kutoka Tanzania walizama majini baada ya gari lao la kijeshi,
kukwama katika mto mmoja nchini Sudan.
Katibu huyo mkuu vile vile alilieleza baraza
hilo kuwa kikosi chake nchini Sudan kinakabiliwa na upungufu wa vifaa
vya kutosha na vya kisasa, hali ambayo inaadhiriwa juhudi zao za kutunza
amani katika eneo hilo la Darfur.
Wanajeshi hao wa Umoja wa Mataifa, wako katika
eneo hilo la Darfur, kujaribu kumaliza mzozo uliodumu kwa miongo kadhaa
kati ya wanajeshi wa serikali na waasi.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu laki tatu wameuawa kwenye mzozo huo wa Darfur
No comments:
Post a Comment