Saturday 29 June 2013

HICHO NDICHO KISA CHA KASEJA KUACHWA NA SIMBA

Photo: Juma Kaseja ONDOKA SIMBA...!!!!1
 
 
 
Japokuwa haija wekwa wazi sababu rasmi ya kuachwa kwa kipa Juma Kaseja, imebainika kwamba ni kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya mahasimu wao Yanga.
Simba ilipokea kipigo hicho, katika mchezo wa funga dimba wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Mei 18 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo Kaseja Ndiye aliyekaa langoni.
 

Habari za kuaminika toka ndani ya uongozi wa Simba zinaeleza kuwa kipigo hicho kiliwakera viongozi wa klabu hiyo kukiwa na madai kuwa kilitokana na uzembe au makusudi.

Kiongozi mmoja wa Simba ameuambia Mtandao huu kuu pamoja na upungufu mwengine ambao kipa huyo amekuwa akihusishwa nao, mazingira ya mabao mawili dhidi ya Yanga, ndiyo yamemwondoa Msimbazi.

“Kaseja ni kipa mzuri, hivi unavyomfahamu anaweza kufungwa mabao kama yale? Kwa kweli hilo limetuacha na maswali mengi kichwani, imetukera sana, mwache aende zake akatafute maisha sehemu nyingine,” alisema kiongozi huyo kwa sharti la kutotajwa jina.

Akienda mbali zaidi, kiongozi huyo alisema ingekuwa vizuri zaidi kama Kaseja angeweza kuonesha umahiri wake na kuondoa dhana mbovu dhidi yake, lakini kitendo cha kukubali nyavu zake kutikiswa kilitoa jawabu juu ya maswali waliyokuwa nayo.

Siku za karibuni kumekuwa na utata juu ya Kaseja kubaki Msimbazi baada ya mkataba wake kufikia mwisho huku akizua mgawanyiko miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Usajili kwa wengine kutaka asajiliwe na wengine wakitaka aachwe.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa klabu hiyo Alhaj Ismail Aden Rage, Kaimu Makamu Joseph Itang’are ‘Kinesi’ na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zakaria Hanspoppe, kwa nyakati tofauti walisema Kaseja hawezi kuongezewa mkataba.

Viongozi hao walitoa kauli hizo bila ya kueleza wazi sababu za kumuacha kipa huyo namba moja wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ambaye ameitumikia klabu hiyo karibu miaka 10.

Hayo yakiendelea, Kaseja mwenyewe  hakuwa tayari kusema lolote, ingawa kuna habari kuwa huenda akatua Coastal Union ya Tanga au Mtibwa Sugar ya Turiani.

Aidha, Yanga imemnasa mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Husssein Javu ambaye pia alikuwa akiwaniwa na Simba.

Habari kutoka Yanga, zinasema nyota huyo amesaini mkataba wa miaka miwili kwa ajili ya kuitumikia klabu hiyo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!