Thursday, 30 May 2013

WANAUME WASINYANYAPAE WAKE WANAPOUGUA FISTULA


WIKI iliyopita ilikuwa ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Utokomezaji wa Ugonjwa wa Fistula.
Katika maadhimisho hayo, wanawake waliopatwa na tatizo hilo walipata nafasi ya kutoa ushuhuda wao kuhusu mahusiano yao na waume zao baada ya tatizo kutokea.
Katika maelezo yao wapo wanawake wachache waliokiri kuwa baada ya kuugua ugonjwa huo walipata ushirikiano kutoka kwa waume zao, wengine walisema walitengwa.
Aidha, mbali na kutengwa na wanaume waliokuwa wakiishi nao, wakati mwingine walijikuta hata watoto waliozaliwa na kusababisha mama zao kupata ugonjwa huo nao walikosa huduma stahiki na kwa wakati kutokana na baba zao kukimbia majukumu yao katika familia.
Maneno hayo yaliyotolewa na baadhi ya wanawake waliotibiwa ugonjwa wa fistula katika Hospitali ya CCBRT na kupona, yanatoa ushahidi kuwa wanaume wanahitaji kuelimishwa zaidi kuhusu ugonjwa huo ili wasinyanyapae wanawake pindi wanapougua.
Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya wanawake 3,000 wanapata tatizo la fistula kila mwaka, hivyo ipo haja ya kuwa na mikakati itakayohakikisha ugonjwa huo unapunguzwa kwa kiwango kikubwa ili kurejesha heshima ya wanawake.
Elimu ya afya ni jambo la muhimu kwa kila upande ambapo itasaidia mlengwa kujua hali ya mwili wake na ni jinsi gani anaweza kupata matibabu ili kumwepusha na matatizo mengine anayoweza kukumbana nayo ambayo kwa upande mwingine yanaweza kumletea ulemavu wa mwili.
Aidha, wapo wanaoishi kwa kuamini dhana ya ushirikina zaidi, jambo ambalo huwaletea madhara zaidi pindi anapougua, kwani hushindwa kwenda kwa wataalamu wa afya na badala yake kujikuta akipoteza maisha ama kubaki na ulemavu ambao ungeweza kupona haraka hospitalini.
Inawezekana wapo wanawake pia ambao wana roho ya unyanyapaa, kutowatia moyo wagonjwa na hata wakati mwingine kwa kujua ama kutojua, jambo ambalo linaweza kuchangia mgonjwa kuona hali aliyonayo haiwezekani kupona na kurejea katika hali ya kawaida.
Kutokana na kuwepo kwa hali kama hiyo katika jamii, ifahamike kuwa sasa ugonjwa huo unatibika na wanawake takribani 1,365 waliokuwa wakipata matibabu katika Hospitali ya CCBRT walipona na kuendelea na shughuli zao za kujenga uchumi.
Ipo haja ya kufikia wanaume kupata elimu zaidi ya jinsi ya kuwa karibu na wanawake, pindi wanapougua fistula, kuwatia moyo, waishi kwa matumaini, kutowanyanyapaa na kutowatenga kwani ugonjwa huo unatibika.
Kadhalika, wanawake wanashauriwa kuwa jasiri wajitokeze pindi wanapoona dalili za magonjwa katika miili yao na hata wakati mwingine kuuliza kwa wengine kwani ugonjwa huo una tiba.
Kutokana na kuwepo kwa matibabu, mbali ya kupata ushirikiano kutoka kwa wanaume, lakini pia wale waliopona wawe mabalozi wa kutoa elimu kwa pande zote kuhusu ugonjwa huo kwani umekuwa ukiwakwaza wanawake na kuonekana kama waliokosa katika jamii.
Kwa mantiki hiyo, ni jukumu la akina baba kuwatia moyo wanawake kuwa ugonjwa huo unatibika, hivyo wasiwatenge wanawake waliougua ila wawatie moyo na waishi nao kwa matumaini bila kukata tamaa.
Kupitia matibabu hayo yanayotolewa CCBRT, wanawake wanatakiwa kutokuwa na hofu kwani hospitali hiyo inatoa huduma ya usafiri kwa wanawake wagonjwa wa fistula kutoka majumbani kwao hadi hospitalini na hivyo kupata matibabu sahihi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!