Pages

Thursday, 1 March 2018

Matukio ya ubakaji na siri kwa wanaobakwa



Image result for ubakaji
KUMEKUWEPO na matukio ya udhalilishaji na ukatili wa wanawake na watoto ambao umesababisha madhara ya kimwili na kisaikolojia. Baadhi yamekuwa yakiripotiwa na mengine kubaki siri kwa waliobakwa kama ambavyo utafiti uliowahi kufanywa unabainisha.

Dk Felix Kisanga kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa na Tiba na Teknolojia (IMTU) anasema upo utafiti uliofanywa kwa miaka minne kuanzia mwaka 2007 hadi 2011 juu ya matukio hayo.
Utafiti huo uliohusisha wataalamu wa masuala ya afya, umeibua mambo mbalimbali ikiwemo suala zima la jamii na waathirika kuyafanya vitendo hivyo siri na hivyo kusababisha wahusika kutochukuliwa hatua.
Katika utafiti wake na wataalamu wengine watatu, Dk Kisanga anasema ulihusisha matukio ya watoto kubakwa na vitu vinavyosababisha hali hiyo.
Wenzake watatu walifanya katika maeneo tofauti ambayo ni matukio ya udhalilishaji kati ya wanandoa, matukio ya kubakwa kwa wanawake pamoja na uelimishaji jamii jinsi ya kuyatambua na utoaji wa taarifa ya matukio hayo ili sheria ichukue mkondo wake.
Anawataja watafiti wenzake kuwa ni Dk Rose Laizer ambaye alifanya utafiti katika eneo la matukio ya udhalilishaji kati ya wana ndoa. Profesa Projestine Muganyizi alifanya utafiti unaohusu matukio ya wanawake kubakwa na utafiti wote ulifanyika katika wilaya ya Temeke, Dar es Salaam.
Utafiti mwingine ulifanywa na Dk Muzdalifat Abeid na ulihusu uelimishaji jamii kutambua na kutoa taarifa ya matukio hayo ili sheria ichukue mkondo wake.
Aliufanyia Kilombero mkoani Morogoro. Watoto kubakwa Kuhusu watoto kubakwa, kwa mujibu wa Dk Kisanga, inaonesha mtoto mmoja kati ya wanne upande wa wasichana, na mtoto mmoja kati ya wavulana watatu wameshawahi kukumbwa na tatizo linalowadhalilisha; la kingono, kijinsia ama kiakili.
“Kwenye utafiti huu ilionekana wahusika wakuu ni majirani, walimu, ndugu na watoto wenzao. Mengi yanayosababisha matukio haya ni umasikini uliokithiri pamoja na ushirikina,” anasema.
Anatoa mfano katika eneo la ushirikina ni kwamba, watu wamekuwa wakitafuta utajiri wanapoenda kwa waganga, kwani wengi wao wanashauriwa wabake mtoto hata yule anayenyonya ili wapate utajiri. Anafafanua kuwa unyanyasaji wa watoto ni tukio lolote la kingono linalomhusisha mtoto ambalo mtu mzima au mtoto mwenziye analifanya ajiridhishe.
“Wanaofanya matukio haya, wanadhalilisha au kurubuni watoto wadogo ambao hawana uwezo wa kukataa lakini katika umri wa kutoa ridhaa hawajafikia,” anasema. Anasema matukio ya watoto kudhalilishwa kingono ni asilimia tatu hadi 16 kwa wavulana na asilimia mbili hadi 62 kwa wasichana katika bara la Ulaya.
“Na kwa hapa Tanzania ni asilimia 13 ya wavulana au 28 kwa wasichana chini ya miaka 18 kutokana na utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), wa mwaka 2009,” anasema.
Anasema katika utafiti wake, upande wa matukio ya udhalilishaji wa watoto walihusishwa mahakimu, polisi, ustawi wa jamii na watu maalumu wenye taarifa hizo zikiwemo wizara husika.
Vile vile walikwenda kwenye shule za sekondari 23 kati ya shule 71 zilizokuwepo. Wakati huo katika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam alizungumza na watoto 1,359, pia kuzungumza na jamii mbalimbali na watoa huduma za afya kuhusu matukio hayo.
Anasema kwa upande wa watoto kubakwa matukio hayo kuripotiwa ni vigumu lakini kunapotokea madhara huwa rahisi kuripotiwa, kwa sababu ni lazima upande wa waathirika utoe taarifa sahihi ili waweze kupata msaada stahili. Akizungumzia upande wa matukio ya udhalilishaji wa wanawake, anasema utafiti uliangalia upande wa wafanyakazi wa afya, na kubaini wengi wa wafanyakazi hao hawana uelewa wa kutosha katika kuwatambua wanawake waliokumbwa na matatizo hayo waendapo kupata huduma.
“Kutokana na hali hii kulitengenezwa kielelezo cha kumsaidia mhudumu ili mgonjwa anapohojiwa ijulikane amepatwa na tukio la udhalilishaji au la,” anasema.
Anasema utafiti ulibaini kwenye eneo la matukio ya ubakaji wa wanawake, wengi hawazungumzi wanabaki nayo mpaka awe na mtu anayemwamini sana ndiye anamwelezea.
Anasema matukio ya wanawake kubakwa Tanzania ni asilimia 12 hadi 20, kwa wanawake wenye miaka 12 au zaidi na asilimia 23 hadi 31 kwa wanawake wale waliowahi kuingia kwenye mahusiano ya ndoa wenye umri kati ya miaka 15 na 49 na hawa wanadhalilishwa na wenzi wao.
Matukio ya kudhalilishwa wanawake yanaripotiwa mikoa hususani ya Mara na Mbeya na maeneo mengine lakini hayo mawili yanazidi asilimia 40. Siri kwa wanaobakwa Matukio mengi yanafichwa; hayaripotiwi kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni kuficha aibu ya aliyedhalilishwa na familia yake.
Mhusika au mdhalilishaji humtishia mtoto kuwa atamuua endapo angefichua jambo hilo. Familia mbili zinazohusika zinaweza kujadili na kuyamaliza kwa malipo.
Baadhi ya watu huendelea kufanyiwa matendo hayo ya kikatili na matokeo yake ni kuathirika kisaikolojia. Je, haki inatendeka? Inaelezwa kuwa baadhi ya matukio hufika kwenye ngazi ya haki lakini mengi hayafiki.
Katika utafiti huo, iligundulika kuwa kujadili na kuyamaliza baina ya familia husika husababisha matukio hayo yasiende mbele kwa lengo la kuchukua hatua. Pia rushwa na polisi husababisha hali hiyo.
“Kwa upande wa mahakama, utafiti unaonesha kuwa waathirika ambao ni masikini kwa kuwa tarehe za kesi zinarushwa mara kwa mara, watashindwa kupeleka mashahidi wao mara nyingi kutokana na ukosefu wa fedha, hivyo watafika mahali watashindwa kuendelea,” anasema.
Pia walibaini kuwa kesi nyingi hucheleweshwa kwa sababu ya uchunguzi kutokamilika. Anasema sheria ya mwaka 1971 inayohusu ndoa, inaruhusu mtoto aliyefika miaka 14 kuolewa, hivyo watu wengi wenye kutaka kubaka watoto wanatumia kigezo hicho.
Kwa upande mwingine sheria ya mtoto ya mwaka 2009 inamtambua mtoto chini ya miaka 18 kuwa yeye ni mtoto anatakiwa kusoma kujitengenezea maisha ya baadaye.
Anabainisha kuwa sheria ya watoto ya 2009 ambayo inamtambua na kumlinda mtoto inakinzana na sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inamruhusu kuolewa.
Anapendekeza kuwa sheria hii ingefutwa kabisa au kufanyiwa marekebisho kuzuia watoto chini ya miaka 18 kuolewa. Akizungumzia matukio ya wanawake kubakwa wengi wao wanakumbwa na matukio hayo kwa asilimia 32. “Asilimia 15 inatokea kwa wanandoa na asilimia 12 yanahusishwa na matumizi ya pombe kwa waathirika”.
Aidha aliongeza kuwa asilimia 99 ya matukio yanajulikana kuwa ni ubakaji endapo yanapofanywa na watu wasiojulikana na mwathirika. Sida imekuwa ikitoa fedha za utafiti kwa vyuo mbalimbali kikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu Ardhi (ARU), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), pamoja na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech).

No comments:

Post a Comment