Pages

Sunday, 25 February 2018

Hofu ya kupima, unyanyapaa vikwazo kumaliza ukimwi

HOFU ya kupimwa virusi vya Ukimwi (VVU), kuanza kutumia dawa za kufubaza virusi (ARVs) na unyanyapaa ni miongoni mwa changamoto katika utekelezaji wa mpango wa 90-90-90 katika suala zima la mwitiko wa VVU na Ukimwi.


Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano yenye kuleta Mabadiliko ya Tabia, kutoka Taasisi ya JHPIEGO, Yeromine Mlawa ameyasema hayo wakati wa kutoa mada kwenye semina ya waandishi wa habari kuhusiana na VVU na Ukimwi na mchango wa tasnia hiyo kufikia malengo ya nchi katika mwitiko wa VVU na Ukimwi.
Amesema, jamii ya Watanzania wamekuwa na hofu katika kupima ili kujua hali zao, hofu inayotokana na dhana kuwa mtu akigundulika kuwa na maambukizi ya VVU ndiyo mwisho wa maisha yake, jambo ambalo si kweli.
"Ukipima na kujua hali yako ya maambukizi ya VVU ni kama umepata bingo, kwa sasa endapo umepima na kukutwa itakusaidia kufanya mwili kuwa na kinga imara dhidi ya magonjwa mbalimbali na kuweza kuendelea na shughuli zao," amesema.
Ametoa mfano utekelezaji wa Mradi wa Sauti katika kuifikia 90-90-90 ifikapo mwaka 2020, Mlawa alisema kuanzia mwaka 2015 mpaka sasa wamepima watu milioni 1.6 na watu 53,000 wakikutwa na maambukizi huku, watu 30,000 wakiazishiwa matibabu.
"Hali ilivyo sasa asilimia 52 ya Watanzania wamepima na kujua hali zao kuhusiana na VVU, mikakati ya sasa ni kuwafikia asilimia 48 iliyobaki hasa kwa kufuatilia mtandao wa watakaotambuliwa kuwa na maambukizi ya VVU," amesema.

No comments:

Post a Comment