Monday, 21 December 2015

HOSPITALI ZAAGIZWA KUTENGENEZA MFUMO WA MALIPO WA KIELEKTRONIKI‏

IMG_9410
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi Kigwangalla akifurahi jambo na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sokoine ya Mkoa wa Lindi, Dkt. Evaristo Kasanga (kulia) wakati wa ziara ya kushtukiza aliyofanya mwishoni mwa juma mkoa wa Lindi.(Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog)


Na Mwandishi wetu, Mtwara
NAIBU Waziri katika Wizari wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla ameagiza kubadilishwa kwa mifumo ya utawala, malipo na uendeshaji katika katika hospitali nchini ili kuleta ufanisi na tija.
Akizungumza katika ziara yake ya kujifunza kuona katika hali ya kawaida huwa zinatolewaje katika hospitali za wilaya na mikoa alisema kukosekana kwa mifumo bora ya malipo na motisha kumedumaza utumishi.
Ziara yake hiyo ambayo aliifanya katika hospitali ya mkoa wa Lindi ya Sokoine na Ile ya Mtwara ya Ligula ililenga kuona masuala mbalimbali yanayohusiana na utoaji huduma ili kuwa na nafasi ya kutengeneza hali bora zaidi kimkakati.
Alisema tatizo la upungufu wa dawa na hata raslimali watu linasababishwa na kukosekana kwa mfumo waukusanyaji mapato ulio sahihi na wenye salama ambao utawezesha pia kutoa motisha mbalimbali kwa watumishi ili kuwavutia kufanyakazi katika mikoa ya pembezoni.
Aidha alisema malipo yanayofanyika katika hospitali hizo yanatakiwa kuwa ya kielektroniki kwa kuwa imethibitishwa kila kunapokuwapo na mfumo wa malipo kielektroniki unaboresha mapato na hatimaye kuboresha ufanisi katika uendeshaji wa hospitali pamoja na kuwapo kwa huduma bora za dawa.
Pia ameagiza kuharakishwa kwa mfumo wa malipo kielektroniki kwa wateja wa Bima ili mchango wao usaidie kwa haraka utoaji wa huduma ndani ya hospitali.
Hata hivyo Naibu Waziri huyo alisema aliridhishwa na utendaji katika hospitali ya Sokoine na Ligula na kusema ufanisi wao unatokana na kuwapo kwa mipango inayowezesha kazi kufanywa.
Alisema hospitali ya Sokoine imeanzisha utaratibu wa mawasiliano ambao unawezesha daktari mahali popote pale kuitwa huku kila mmoja akijua kwamba daktari ameitwa eneo Fulani.
Alitaka hospitali nyingine nchini hasa za rufaa kuangalia mfumo wa mawasiliano ya ndani wa Hospitali ya Sokoine ili kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Pia alipongeza utendaji wa hospitali ya Ligula na kusema kwamba kutokana na ufanisi wao na huduma nzuri ndio maana hata wananchi wa nchi jirani wanafika katika hospitali hiyo kupata huduma.
Alisema kama kusingelikuwa na huduma bora wananchi hao wasingelivuka kuja kutafuta huduma Ligula.
Hata hivyo Naibu Waziri huyo alitaka kuwapo na utaratibu wa kudhibiti hali hiyo na kusema kwamba ni matumaini yake kuwa wataalamu wataketi pamoja na kutafuta namna ya kufanya katika mazingira hayo ya pia kuhudumia raia wa nchi jirani.
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Ligula ya mkoa wa Mtwara, Dkt. Shaibu Maarifa, alisema kwamba pamoja na huduma wanazotoa wanakabiliwa na changamoto kadha hasa wodi ya wanawake na wajawazito.
Alisema kutokana na ongezeko la watu katika mji wa Mtwara kutokana na kuwapo kwa fursa kubwa za uchumi wa gesi na kiwanda cha saruji cha Dangote, wafanyakazi wamekuwa wakifika na familia zao na hivyo kwa sasa wodi hiyo haitoshi.
Hata hivyo alisema hali ingekuwa mbaya zaidi kama kituo cha afya cha Lipombe kisingesaidiana na hospitali hiyo.
Alisema wodi ya watoto kwa sasa inafanyiwa ukarabati na benki ya Eco na wana mkakati mwingine wa kuomba msaada wa kuondoa ufinyu wa wodi ya wanawake.
Alisema anashukuru Katibu Tawala wa mkoa wa Mtwara, Alfred Luwanda na Mkuu wa mkoa wameshafika katika hospitali hiyo na wameahidi kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba matatizo yake yanatatuliwa na kukidhi hospitali ya rufaa.
Kuhusu upatikanaji wa dawa alisema kwamba hospitali hiyo wa sasa ina akiba ya kutosha baada ya serikali kuipelekea sh milioni 80 na tayari wameshazilipa kwa Bohari ya Dawa (MSD).
Aidha alisema dawa za bima afya zipo na kwamba hawatarajii tatizo kwa kuwa wamekubaliana na mamlaka husika kukitokea upungufu watatumia hata fedha za bima kwa ajili ya kupunguza upungufu wa dawa.
Hata hivyo alisema kwamba wanakabiliwa na uhaba wa madaktari bingwa kwani kwa sasa wana dakatri bingwa wa mifupa na wanawake.
IMG_9338
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi Kigwangalla akipewa maelezo na Kaimu Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Sokoine ya Mkoa wa Lindi, Damasiana Msalla alipotembelea wodi ya wazazi na kuridhishwa na huduma za hospitalini hiyo wakati wa ziara ya kushtukiza aliyoifanya mwishoni mwa juma mkoani Lindi.
IMG_9435
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sokoine ya Mkoa wa Lindi, Dkt. Evaristo Kasanga akizungumza jambo na Eleuteri Mangi, Afisa kutoka Idara ya Habari -MAELEZO jijini Dar es Salaam.
IMG_9423
Hospitali ya Sokoine ya Mkoa wa Lindi imetwaa kombe la mshindi wa pili kwa utoaji wa huduma bora Tanzania kwa mwaka 2015.
18
Jedwali linaloonesha baadhi ya gharama za matibabu katika huduma zinazotolewa hospitali ya Sokoine ya Mkoa wa Lindi.
IMG_9349
Ujumbe wa watoa huduma kwa wateja wanaofika kupata huduma hospitali ya Sokoine ya Mkoa wa Lindi.
IMG_9572
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi Kigwangalla (katikati) akiongozana na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Ligula ya mkoa wa Mtwara, Dkt. Shaibu Maarifa (kushoto) pamoja na Daktari wa zamu kitengo cha dharura hospitalini hapo, Dkt. Ester Tumwanga kuelekea wodi za wagonjwa wakati wa ziara ya kushtukiza aliyofanya mwishoni mwa juma mkoani humo.
IMG_9525
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi Kigwangalla akiwa kwenye chumba cha dharura katika Hospitali ya Ligula ya mkoa wa Mtwara. Kushoto ni Daktari wa zamu kitengo cha dharura hospitalini hapo, Dkt. Ester Tumwanga.
IMG_9606
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi Kigwangalla akitoka kwenye wodi ya wazazi Hospitali ya Ligula ya mkoa wa Mtwara wakati wa ziara ya kushtukiza aliyofanya mwishoni mwa juma mkoani humo. Aliefuatana nae ni Mganga Mkuu wa Hospitali ya Ligula ya mkoa wa Mtwara, Dkt. Shaibu Maarifa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!