Saturday, 24 January 2015
WATOTO KUFANYISHWA BIASHARA KWENYE VITUO VYA MABASI NANI ALAUMIWE?
Haya ndiyo maisha ya watoto wengi wanaozagaa kwenye stendi za daladala jijini Dar es Salaam. Katika kituo cha Mbezi Luis au Mbezi stendi mpya mara nyingi jioni kuna kusanyiko la watoto kituoni wakiuza bidhaa hasa sigara, karanga, ubuyu, kashata na matunda.
Kinachojiri ni watoto hawa wadogo wenye miaka chini ya 10 kujikuta wako karibu na majirani wenye vurugu ama ‘wasio na maadili’ ambao ni wapiga debe, madereva wanaoendesha kwa kasi magari yanayotoa moshi na kelele nyingi, wavuta unga na wanywa pombe za viroba wanaoongea matusi ya nguoni ambayo ni lugha inayoathiri tabia na ukuaji wa watoto.
Watoto hawa wanakusanyika eneo hilo jioni wakati mwingine wako peke yao ama na wazazi au jamaa wengine lakini hili haliwazuii kusikia maneno machafu kutoka kwa majirani hao wasio na maadili. Pia haliwakingi na athari za moshi wenye sumu.
Zamani ilikuwa wazazi wanawafungia watoto wao majumbani ama wanawakabidhi kwa majirani kucheza nao lakini hilo sasa linashindikana ndiyo maana wanakwenda nao vituo kwenye mazingira mabovu kiafya kimalezi kwani hakuna usalama wanapowaacha nyuma.
Wanashindwa kuwaacha nyumbani ama kwa marafiki kwa kuhofia kuwa watabakwa ama kunyanyaswa kingono kwa sababu ya ukatili dhidi ya watoto uliokithiri mitaani na wakati mwingine ukifanywa na ndugu ama majirani wa karibu.
Katika mahojiano na baadhi ya wazazi kituoni Mbezi wanataja ugumu wa kuwaacha watoto nyumbani wanaokutana nao. Huo ndiyo unaowalazimisha kufika pamoja nao kwenye kituoni ambako si mahali salama hasa nyakati za jioni.
Maliga Musika ni mama ni watoto wawili wenye miaka tisa na 12 ambao anakuwa pamoja nao kuuza sigara ,ubuyu na karanga katika kituo hicho.
Ananieleza kuwa anafahamu kituoni hapo si mahali salama kwa watoto akitaja uwezekano wa kupata magonjwa ya ngozi.
“Wachanga hao ngozi zao ni laini wanaweza kupata magonjwa ya upele na mzigo (aleji) . Kwa kifupi ni tishio la afya kwa watoto hawa wadogo,” anasema Musika na kueleza kuwa kuna hofu ya kupata maradhi ya njia za hewa miongoni mwa watoto hao wadogo.
Anasema tatizo linatokana na magari pamoja na boda boda kupumua moshi mzito unaoweza kuwadhuru. “Hewa hii chafu wanayovuta inawaathiri lakini ndivyo hali ilivyo eneo hili. Maisha ni magumu ni lazima kuwashirikisha kutafuta chakula chao,” anajitetea Musika, ambaye ni mama wa watoto wane.
Watoto wanasikia matusi yanayozungumzwa na wakaaji wa stendi ambao ni pamoja na wavuta unga, wapiga debe na makondakta. Kelele nyingi zinasababishwa kuumwa kichwa na hata kuharibu hali ya utimilifu wa masikio, anaeleza daktari jirani wa hospitali ya KIpasika iliyoko karibu na kituo cha Mbezi.
Anasema kuwaacha watoto kwenye kelele hizo kwa muda mrefu kutawasababisha matatizo ya usikivu siku za usoni na pia kunasababisha kuumwa kichwa mara kwa mara.
“Familia nyingi zinazofanya biashara hapa pamoja na watoto wao hazina uwezo kununua dawa hata za kutuliza maumivu.Mathalani mtoto anapoumwa na kichwa, mafua au macho inakuwa vigumu kumtibu.Ni tatizo kunahitajika kuwapa ushauri na elimu zaidi wazazi hawa” anasema Dk huyu anayeomba jina lake lisiandikwe.
Lakini pia karibu na stendi hiyo kuna kanisa ambalo waumini hukusanyika kwenye Hema ya Bwana. Baadhi yao wanaeleza kuwa kuwafikisha watoto wadogo kwenye biashara nyakati za usiku, kunawazuia kujisomea, kucheza na hata kula na kulala kwa wakati.
Wanaeleza wasiwasi wao kuwa kuwaingiza kwenye biashara mapema kunaweza kuwafanya wasipende kusoma na kujikita zaidi kwenye maisha ya utafutaji jambo ambalo si baya lakini lilipaswa kufanywa baada ya kumaliza masomo tena kitaalamu badala ya hali ilivyo sasa.
Baadhi ya wadau wanaotetea haki za watoto walipendekeza katika katiba mpya kuwe na msingi utakaolinda haki za watoto , ikiwawezesha kupata huduma za elimu, kuwalinda dhidi ya ukatli wa kijinsia na kwa watoto wa kike kuepushwa na ndoa za utotoni.
Pengine katiba mpya itakuwa dawa ya kuzia utumikishwaji watoto wadogo pia kuwakuta wakizagaa mitaani na maeneo hatarishi kwenye stendi za mabasi zenye majirani wasio na maadili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
aziz bilal17:09
1
Reply
Hapa ni serikali ndio walaumiwe,wazazi ajira hawazipati hata kitu inaitwa job creation haijulikani ilipotelea mitaa gani wanashindwa hata kiwanda cha nguo na ilhali pamba tunayo ya kutosha,hii ni aibu kubwa kwa serikali yetu.
Post a Comment