Saturday, 26 October 2013

JK:RUSHWA ITAIZIKA CCM


Mwenyekiti wa CCM taifa, Rais Jakaya Kikwete.
RAIS Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amesema tatizo la rushwa ndani ya chama hicho lisipodhibitiwa litakiondoa chama hicho madarakani.
Amesema chama hicho kikishinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na tatizo la rushwa likaendelea, litakifanya chama hicho kutoshinda tena katika uchaguzi wa mwaka 2020.
“Tukiendelea hivyo, tukishinda uchaguzi ujao wa mwaka 2015 ni bahati, lakini tukifanikiwa kupenya uchaguzi wa mwaka 2020 hatutoki,” alisema.
Alisema hayo juzi mjini hapa wakati akifunga mafunzo maalumu ya watendaji wa wilaya na mikoa wa CCM na kumpa rungu Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phillip Mangula kuwashughulikia viongozi wala rushwa ndani ya chama hicho.
“Tusipoangalia hili la rushwa tutaiondoa madarakani CCM na mambo yote mazuri tuliyofanya hayataonekana, hapo lazima wananchi watawauliza je, ugonjwa huu mmeshindwa kuachana nao, basi tumeamua kuwapumzisha,” alisema.
Mwenyekiti wa chama hicho kilicho madarakani tangu Tanzania ipate uhuru, alisema rushwa itaizika CCM kwani hiyo ni hila ambayo itakifanya chama hicho kishindwe kuongoza kwa muda mrefu.
“Acheni kuvutavuta, mtu anarushiwa Sh 200,000 ya air time (muda wa maongezi wa simu ya mkononi) hiyo ni nini acheni hicho kitu,” alisema na kuongeza kuwa tatizo la rushwa limewachosha wananchi na kutishia chama kuendelea kuongoza.

Alisema wanaotoa fedha ndio wanapokewa kwa shangwe na viongozi hao ndio wamekuwa wakiwatafutia watu ushindi, kitu ambacho wananchi wamekichoka na kuwa na chuki na chama hicho.

“Nakupa Mangula (Phillip) rungu la kuhangaika nao,” alisema Rais Kiwete huku akishangiliwa na wajumbe hao wa mkutano.
Alisema dawa ya viongozi kama hao ni kuachana nao kwani kuna makada wengi ambao hawana makandokando lakini wale wenye maradhi hayo chama hakiwezi kuendelea nao.

“Njaa taabu sana, ukiendekeza sana njaa ndiyo inakuwa hivyo, utu unakutoka, tusifanye hivyo chuki ya watu kwa rushwa ni kubwa, kiongozi kuwa wakala wa kusambaza fedha ni aibu kama unatosha utapita tu,” alisema.

Alisema mafunzo hayo yatasaidia kuweka sawa ng’we ya pili ya awamu ya nne ya serikali ya CCM na kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya ushindi ni hakika katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2014 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!