INAUMA sana! Mtuhumiwa wa unyongaji wa mwanamke aliyeelezwa kuwa ni mke wa kigogo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Ana Mbago amenaswa kufuatia tukio hilo la kikatili.
Katika tukio hilo lililojiri kwenye makazi ya mama huyo huko Tua-Ngoma, Kigamboni jijini Dar hivi karibuni, anayedaiwa kuhusika na tukio hilo alitajwa kwa jina la Nassoro Kassim (22) hivyo polisi kulazimika kumsaka kwa mauaji hayo ya kinyama kisha kumnasa.
Habari za kiuchunguzi katika eneo la tukio zilidai kuwa kijana Nassoro alikwenda nyumbani kwa mama huyo majira ya saa 3:00 usiku lakini hakukuta mtu kwani alikutana na kufuli mlangoni.
Taarifa ambazo hazina shaka zilieleza kuwa kijana huyo baada ya kubaini hivyo aliamini mama huyo lazima atarudi kwake kulala hivyo alitumia mbinu anazozifahamu na kuingia ndani kwa ajili kumsubiri.
Majirani wa eneo hilo ambao hawakutaka kutajwa walianika mchezo mzima ulivyokuwa kwa kuwaonesha waandishi wetu namna mtuhumiwa huyo alivyoingia ndani kupitia kwenye paa kisha kwenda kutekeleza azma yake.
Inadaiwa kuwa baada ya kuona hakuna mtu kwa nje alipanda ukuta kimafia hadi juu kwenye paa kisha kutoboa sehemu na kuingilia kwenye ‘silingibodi’, akazama ndani na kujificha sehemu. Ilikuwa kama muvi vile!
Ilisemekana kuwa mtuhumiwa huyo alitulia ndani hadi mwanamke huyo alipofika na kufungua nyumba yake bila wasiwasi akijua kuwa yuko peke yake.
Baadaye mama huyo alifunga milango yake kwa loki za kawaida na kufuli.
Mashuhuda hao ambao ni majirani, walidai kuwa wakati huo ilikuwa saa 4:00 usiku ambapo mama huyo alikuwa amerejea na chipsi lakini wakati anaanza kula tu ndipo mkasa ulipomkuta.
Ilidaiwa kuwa ghafla kijana Nassoro alijitokeza na kumvaa kwa kumkaba koo huku mama huyo akipiga kelele kuomba msaada.
Iliendelea kusemekana kuwa katika purukushani hiyo, Nassoro alisikika akimwambia atoe fedha lakini mama huyo alikuwa ameishiwa nguvu.
Kutokana na kelele za mwanzo za mama huyo ambazo baadaye zilizima ghafla zilisababisha majirani na sungusungu kufika lakini waliogopa kuvunja mlango kwa madai kuwa watakuwa wamekwenda kinyume na utaratibu hadi polisi wafike huku ikidaiwa kulikuwa na kitu nyuma ya pazia.
Jeshi la polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke lilifika eneo la tukio kwa muda mwafaka usiku huo ambapo walivunja mlango na kumkuta Anna akiwa bado hai, amelala sakafuni lakini hana nguvu huku mtuhumiwa akiwa haonekani.
Polisi walimchukua Anna kwa lengo la kumkimbiza hospitali kisha kumsaka mtuhumiwa huyo lakini wakiwa njiani walitoa taarifa kuwa mgonjwa waliyemchukua alikuwa amefariki dunia.
Baada ya kukamatwa maeneo hayohayo ya Tua-Ngoma, mtuhumiwa huyo aliwashangaza watu baada ya kutoa ushuhuda kuwa ni mara yake ya kwanza kuua huku akiwa hana silaha yoyote, jambo lililoashiria kuwa alimnyonga mama huyo aliyeonekana na alama ya kukabwa shingoni.
Kwa upande wake, mume wa marehemu ambaye ni afisa mwandamizi katika Benki Kuu ya Tanzania, Joseph Mbago alikiri kuwa hakuwepo nyumbani hapo na kusema kuwa alikuwa kwa mke mdogo ambapo alipata taarifa hizo kwa njia ya simu na kuamua kwenda usiku huo huko Tua-Ngoma.
Alisema baada ya kufika alikutana na umati mkubwa wa watu na kuamini kuwa simu aliyopigiwa ilikuwa na ukweli hivyo akapigwa na butwaa.
“Siamini kama kweli Anna wangu kafariki dunia kwa kunyongwa,” alisema Mbago huku machozi yakimtoka.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke, Engelbert Kiondo alisema kuwa kijana huyo alifanya tukio la kinyama lakini pia alitaka wananchi kuwa na umoja kwani wangeweza kubomoa nyumba ile na kumuokoa mama huyo.
Mtuhumiwa huyo ambaye gazeti hili lilimshuhudia, anashikiliwa na jeshi la polisi huku mwili wa marehemu ukikabidhiwa kwa ndugu kwa mazishi.