Sunday, 7 June 2015
VIFO VINGI VINATOKANA NA KUTOZINGATIA VIWANGO
Ajali na maradhi yatokanayo na ulaji pamoja na unywaji wa vyakula ambavyo vipo chini ya viwango athari zake huchukua muda mrefu.
Wadudu wa maradhi husika wakishajiimarisha mwilini, matokeo yake ni vifo vya ghafla na mara nyingine huwapo maradhi yasiyokubali dawa wala chanjo, yote ni matokeo ya wafanyabiashara wanaokiuka masharti ya kufuata kanuni za viwango.
Mwishoni mwa mwaka jana, nilishuhudia wafanyabiashara ya nguo maarufu kama mitumba walioko kituo cha zamani cha mabasi cha Mwenge jijini Dar es Salaam, wakiuza nguo za ndani ambazo TBS walishapiga marufuku kuwa kiafya hazifai.
Wiki mbili zilizopita, TBS kwa kushirikiana na mamlaka nyingine, iliweza kuteketeza shehena kubwa ya nguo za ndani za mitumba katika dampo la Pugu lililoko nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, ikiwa ni hatua moja muhimu katika kuhakikisha bidhaa za aina hizo hazitumiki tena.
Pamoja na tahadhari zilizotolewa kwa matumizi ya nguo hizo za ndani, bado wafanyabiashara hao wanakaidi na kujifanya hawajui sheria zilizopo, athari ya nguo hizo ni pamoja na kuambukiza magonjwa ya ngozi, uwezekano wa kupata kansa nk.
Kukosekana kwa ajira nchini kisiwe kigezo cha kukiuka taratibu na sheria, kumejitokeza wimbi la wafanyabiashara wasiojali kufuata kanuni, na ndio maana utakuta baadhi yao wametandaza nyanya, vitunguu, matunda nk barabarani wakati pembeni yake kuna maji machafu yanayotiririka.
Tumeingia mwaka huu wa 2015 kwa matarajio mengi, tunaweza kuwa tunatathmini viwango vya afya zetu bila kukumbuka kuwa vigezo vya kuzingatia vilivyowekwa kisheria havizingatiwi.
Wakati huu, tunapopambana na umaskini uliosambaa miongoni mwa sehemu kubwa ya Watanzania, ni lazima pia tuangalie na mchango wa taasisi za serikali pamoja na zile za binafsi ambazo pia zimesaidia kuimarisha afya za wananchi.
Tumesikia namna hatua mbalimbali zilivyochukuliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) zikiwamo kuangamiza shehena za vipodozi vilivyopigwa marufuku, kuzuia matumizi ya madawa ya binadamu ambayo yaligundulika kuuzwa kwa wananchi alihali yalipita muda wake wa matumizi (expiry date), na shehena za nafaka nyingine ambazo hazikufaa kwa matumizi nk.
Moja ya vyanzo vinavyosababisha maafa kwa Watanzania wengi hapa nchini ukiacha magonjwa mbalimbali, ni pamoja na ajali za barabarani, nyingi kati ya hizo husababishwa na uzembe wa madereva wa kutokujali sheria za barabarani, mwendo kasi pamoja na ubovu wa magari.
Kutokana na kasi ya uingizaji magari yaliyotumika nchini, na uwezo wa TBS wa kufanya ukaguzi wa magari hayo, Shirika hilo, mwaka huu liliingia mkataba na Chuo cha Usafirishaji ili kupanua wigo wa ukaguzi wa magari yanayoingizwa nchini kutoka nchi ambazo hazina mawakala wa ukaguzi.
Kwa kipindi kirefu sasa, magari yaliyokuwa yakikaguliwa kabla ya kuingizwa nchini ni yale tu yaliyokuwa yakitoka nchi za Japan, Dubai na Uingreza ambako TBS lina mawakala wake.
Hata hivyo Shirika hilo lilitangaza tenda kwa wengine wanaohitaji kuwa mawakala ili kuongeza nguvu ya uhakiki wa magari kabla hayajaingizwa nchini.
Wafanyabiashara wengi sasa ni wajanja, hasa wale wa nchi za nje ambao wanatumia mbinu nyingi kuhadaa ubora wa bidhaa walizonazo, na ndio maana wananchi wengi huchagua baadhi ya bidhaa zinazotengenezwa kutoka baadhi ya nchi tu wakiamini kuwa ni bora zaidi kuliko za nchi nyingine.
Tanzania ni moja ya nchi zinazoagiza magari mengi kila mwaka kutoka nchi za nje, na kasi yake inafanana na uwiano wa ajali zinazotokea nchini kila kukicha, tunaweza kuamini kuwa uzembe wa madereva ni sababu kubwa ya ajali, lakini pia wingi wa magari yasiyo katika viwango huchangia.
Hatua madhubuti za kupambana na ajali za magari zikizingatiwa, na hasa ukaguzi wa magari wa kila mara utakaozingatia uimara na ubora wa magari husika, kwa dhahiri ajali zinaweza kupungua kwa kiwango kikubwa nchini.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Viwango (TBS), Profesa Cuthbert Mhilu, ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliwahi kusema kampuni ya magari ya East Africa Automobile Services Ltd (EAA) imepewa mkataba mpya wa ukaguzi wa magari yaliyotumika.
Profesa Mhilu alisema EAA wanatumia teknolojia ya hali ya juu wakati wa kufanya ukaguzi ili kuhakikisha Watanzania wanapata magari bora kulingana na thamani ya fedha yao, na akasema hilo wanalisimamia kidete ili kuhakikisha kuwa magari yanayoingizwa nchini yana ubora wa kuridhisha.
Tunaamini Serikali kwa kipindi kirefu imeliona tatizo la ajali nchini, na kwamba inalifanyia kazi ili kupata ufumbuzi wa kudumu, tunaamini pia kila Mtanzania atashiriki kwa njia moja au nyingine kuhakikisha anatoa mchango wake kwa jamii namna ya kudhibiti ajali zinazosababisha kupotea kwa maisha ya ndugu zetu kila wakati, ikiwa ni pamoja na kukemea madereva wanaoendesha magari kwa mwendo kasi bila kuchukua tahadhari.
Wafanyabiashara wa magari ya kusafirisha abiria wazingatie viwango vya ubora wa mabasi wanayoyanunua, wasiangalie unafuu wa bei bila kuangalia uimara wake, pia wawe na viwango maalumu vya sifa za madereva wanaowaajiri, tunaweza kupunguza vifo kwa kiwango kikubwa kama tukizingatia masharti.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment