Wednesday 14 November 2018

Mgambo washikiliwa kwa kupiga na kuua

Picha
POLISI mkoani Kagera inawashikilia askari wa jeshi la akiba (mgambo) wawili, wakazi wa Kijiji Nyakahita wilayani Karagwe kwa tuhuma za kumpiga na kumuua mwanakijiji wakimtuhumu kuingilia majukumu yao ya kazi.



Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Revocatus Malimi aliwataja mgambo hao ni Jackson Kasenene (36) na Paul Berebera (26), wakituhumiwa kumuua Daud Rwenyagira (60) mkulima mkazi wa Nyakahita, Novemba 11, mwaka huu.
Kamanda Malimi alisema mgambo hao walifika kijijini hapo kumkamata Theophili Pima ambaye alichukua fedha kutoka kwa Mali Byamanyirwohi kwa ajili ya kununua kahawa kwa wakulima maarufu kama butura.
Alisema walipofika kumkamata mtu huyo, Rwenyagira aliwasihi wasimkamate kwani siku hiyo ilikuwa Jumapili na kuwaambia ametoka kanisani ni vyema wakarudi siku iliyofuata, jambo lililosababisha mgambo hao kumpiga ngwala na kumkanyaga kifuani kwa madai anaingilia majukumu yao hadi kusababisha kifo chake.
Alisema mgambo hao walikuwa wanatekeleza amri ya Mtendaji wa Kijiji aliyepelekewa malalamiko na Mali Byamanyirwohi aliyetaka kurudishiwa fedha zake na mnunuzi aliyetakiwa kununua kahawa kwa wakulima badala yake akatumia fedha hizo kwa manufaa binafsi.

Na Diana Deus, Bukoba

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!