Monday, 11 June 2018

Samia- Kila Mtanzania awe na bima ya afya

SERIKALI imekiri kuwa huduma za matibabu ni gharama na kuwataka Watanzania kukata bima ya afya ili kupata matibabu ya kibingwa kwa gharama nafuu.

Hatua hiyo imekuja baada ya wananchi waliokwenda kuwaona wagonjwa katika Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MAMC) iliyopo Mloganzila, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, kueleza changamoto za huduma ya matibabu hospitalini hapo.
Wananchi hao walitoa malalamiko yao jana mbele ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, kwamba wamekuwa wakitozwa gharama kubwa za matibabu ikiwemo kulazwa, kutoa maiti, malipo kwa watoto pamoja na ucheleweshwaji wa huduma kutoka kwa madaktari.
Mkazi wa Mbezi, Aisha Ally alisema wanawake wanaojifungua kwa upasuaji baada ya wiki wanapewa bili ya Sh 900,000 kwa mtoto mchanga na mama aliyejifungua kulipa Sh 600,000, hivyo wanaomba zipungue kwa wazazi.
Aisha alisema watu wamekuwa wakiacha maiti zao kwa sababu wanatakiwa kulipa gharama ya Sh milioni sita ili kutoa maiti na kwa sababu ya hali ya maisha, mtu anaamua kutelekeza maiti hiyo.
Ally Mohammed alisema madaktari hawatoi huduma kwa wakati kwa mgonjwa kuachwa kwa siku nzima, bila kupatiwa dawa wala dripu na kusababisha wanapoondoka hawajui kama mgonjwa wao ametibiwa ama la.
“Sisi ni walalahoi tunatoka mikoani na unapoleta mgonjwa hapatiwi matibabu. Wazee wana umri wa miaka 60 wanapewa huduma kwa gharama kubwa, lakini ule msamaha ambao serikali umekuwa ukisema hakuna, watoto wa chini ya miaka mitano pia wanalipia tunaomba muangalie mtusaidie sisi wanyonge,” alisema Mohammed.
Akijibu hoja hizo, Makamu wa Rais alisema kuwa kila Mtanzania anapaswa kuchangia huduma za matibabu na kwamba ili kuepuka gharama kubwa wanatakiwa kuwa na bima ya afya.
“Tunashangaa mnaweza kuchangia huduma nyingine ikiwemo kununua 'vijora' na madera kila wiki ili mwende kwenye sherehe, lakini kukata bima ya afya ambayo unaweza kupata huduma za matibabu kwa mwaka mzima hamtaki. Niwaombe mkate bima ili kuondokana na usumbufu unaojitokeza,” alisema Samia.
Aidha, aliongeza kuwa mambo ya kisera watayafanyia kazi na kwamba inahitajika ushirikiano baina ya serikali na wananchi ili kuboresha sekta ya afya. Alisisitiza kuwa endapo wananchi watakuwa na bima ya afya hawataona gharama kubwa na mtu akitaka kuja mwenyewe hospitali bila rufaa, ni lazima apate bili kubwa za matibabu hivyo suluhisho kubwa ni kuwa na bima.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema ni lazima Watanzania watambue kuwa matibabu ya kibingwa ni gharama, hivyo wahakikishe wanakuwa na bima ya afya ili wapate huduma hizo kwa urahisi.
Aidha, alisema mpaka sasa kuna upungufu wa vitanda 649 pekee kwa Mkoa wa Dar es Salaam na kwamba wanakaribia uwiano wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
“Kwa mujibu wa WHO inaelekeza kila kwenye watu 1,000 kuwe na kitanda kimoja na kwa Dar es Salaam kuna watu zaidi ya milioni tano inatakiwa vitanda 5,000, lakini kwa sasa tunavyo 4,351 ukijumuisha na vya Mloganzila,” alisisitiza waziri huyo.
Mtendaji Mkuu wa hospitali hiyo, Profesa Said Aboud alisema gharama za matibabu za hospitali hiyo, hazitofautiani na za Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH). Alisema wapo wagonjwa waofika wenyewe hospitali hapo ambao ni lazima gharama zao ziwe tofauti na wale wa rufaa kutoka hospitali mbalimbali.
“Nikuhakikishie kuwa katika kipindi cha miezi mitatu tumetoa msamaha wa shilingi milioni 115 kwa wagonjwa waliokuja wakashindwa kulipa huduma za afya kwa mujibu wa taratibu kama mtu amekuja bila kukata rufaa na kutaka kuonana na daktari, kuna gharama za matibabu, vipimo na ushauri na kama hakidhi vigezo vya kusamehewa hawezi kusamehewa,” alifafanua Profesa Aboud.
Kwa mujibu wa mtendaji huyo, wapo baadhi ya wagonjwa wanaofika hapo na kutaka kufanyiwa vipimo kama mgonjwa wa kujitegemea na baadaye wanapopelekewa bili, wanasema hawana uwezo wa kulipa, hivyo wakiendelea kuruhusu hali hiyo hospitali haitaweza kujiendesha.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!