Tuesday, 5 June 2018

Pacha Maria, Consolata kuzikwa Jumatano Tosamaganga

KIKAO kilichofanyika leo Mjini Iringa kimeamua kuwa pacha walioungana, Maria na Consolata Mwakikuti waliofariki dunia mwishoni mwa wiki iliyopita watazikwa Jumatano wiki hii.


Aidha, imekubalika kuwa Maria na Consolata wazikwa katika makaburi ya viongozi wa dini, Tosamaganga yaliyopo nje kidogo ya Mji wa Iringa.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Richard Kesesela amesema, kifo cha wasichana pacha walioungana, Maria na Consolata ni msiba wa kitaifa.
Kwa mujibu wa mwakilishi huyo ambaye ndiye Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mjini,  sababu za kuzika Jumatano ni kutoa mwanya kwa viongozi wa dini wakiwepo maaskofu waweze kuhudhuria.
DC Kasesela amesema Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amethibitisha kushiriki kwenye mazishi ya wasichana hao waliokuwa wakisoma Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha (RUCU), Iringa.
Ameongeza kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Anthony Mavunde pia atakuwepo kwenye mazishi hayo.
“Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dk. Tulia Ackson leo amepita kutoa pole kwa familia ya wafiwa na amesema akipata nafasi atashiriki kwenye mazishi ya wasichana hao,” Kasesela amewaambia wanahabari.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!