Monday 26 March 2018

Wanaume kuhamasishwa wapime ukimwi

TUME ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) inatarajia kuzindua mkakati wa nne wa Taifa Juni mwaka huu, ambao pamoja na mambo mengine unalenga kuwa na kampeni maalum kwa ajili ya kuhamasisha wanaume kupima Ukimwi.


Hatua ya Tacaids inatokana na utafiti uliofanywa mwaka 2016/17, ambao ulibaini kuwepo na mwamko na idadi ndogo ya wanaume katika kupima Virusi vya Ukimwi(VVU) na kutumia dawa za kufubaza makali ya virusi hivyo(ARVs).
Hayo yamebanishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids, Dk.Leonard Maboko alipokuwa akitoa maelezo kuhusu ugonjwa huo na mikakati ya kupambana nao kwa Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi.
Dk. Maboko amesema, utafiti huo ulibainisha maambukizi mapya kwa watu wenye miaka 15-64 ni asilimia 0.29 na kwa wanawake ni 0.40 na wanaume ni 0.17.
Amesema, kwa upande wa kufubaza VVU kwa miaka hiyo ni asilimia 52, ambapo wanawake ni asilimia 57.5 na wanaume ni asilimia 41.2.
"Idadi hii tunaona wanawake ndio wenye utayari wa kupima na kuanza dawa za kufubaza tofauti na wanaume,"alisema.
Amesema, utafiti huo umeonesha kuwa wastani wa maambukizi mapya kwa mwaka ni watu wazima 81,000, ambapo ni sawa na watu 225 kwa siku. Akizungumzia malengo ya tisini tatu, Dk.Maboko alisema katika tisini ya pili na ya tatu Tanzania inafanya vizuri.
"Tisini ya kwanza kwa wanaoishi na virusi vya ukiwmi kujua hali zao ni asilimia 52, katika tisini ya pili ya wanaojua wanatumia dawa(ARV) ni asilimia 90.9 huku tisini ya tatu ambayo ni ya wanaotumia dawa wamefubaza VVU ni asilimia 87.7,"amesema.
Kuhusu hali ya kifedha, alisema mahitaji ya Taifa ya kugharamia Ukimwi yanakadiriwa kufikia Sh.Trilioni 6 kwa kipindi cha miaka 5 ya mkakati.
Alieleza kuwa asilimia 93 ya gharama za Ukimwi kwa mwaka zinafadhiliwa na wadau wa maendeleo kutoka nje ya nchi ikiwemo Serikali ya Marekani kupitia PEPFAR na Mfuko wa Dunia wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria ambao unachangia kwa asilimia 86 huku wadau wengine wakichangia asilimia 7.
Aidha amesema, malengo ya Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi(ATF), ni pamoja na kuongeza mchango wa serikali kufikia Sh bilioni 300 kwa mwaka 2018/19.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye ulemavu Jenista Mhagama, alisema mwaka 2015 serikali ilibaini wafadhili kupunguza kuchangia fedha za mradi ya Ukimwi na hivyo kulazimika kufanya mabadiliko ya sheria ya Ukimwi ambayo iliwekewa kifungu kitakachoanzisha ATF.
Amesema mwaka 2017 mfuko huo ulianza rasmi, ambapo wadau mbalimbali wameanza kuchangia fedha ikiwemo serikali imetenga Sh bilioni 3 mwaka 2017/18.
Hata hivyo, amesema Tacaids imepeleka mapendekezo serikalini kwa ajili ya kuanzisha tozo, itakayowezesha kupatikana fedha kwa ajili ya mfuko huo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge, Oscar Mukasa alisema kamati hiyo ipo tayari kushirikiana na serikali, kuhakikisha malengo ya mfuko huo yanatimia.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!