Tuesday, 27 March 2018

Safari ya kutambua kila mtoto yaendelea

CHETI cha Kuzaliwa ni nyaraka ya msingi ambayo kila mwananchi aliyezaliwa katika eneo la Tanzania Bara anatakiwa kuwa nayo kwani imebeba taarifa nyingi za msingi ambazo humtambulisha aliye nacho.


Katika hali ya kawaida, Cheti cha Kuzaliwa huonekana kama karatasi ya kawaida, lakini ni vyema kila mmoja kutambua kwamba hii ni zaidi ya karatasi.
Umuhimu wa Cheti cha Kuzaliwa huanza kujidhihirisha pale mwananchi anapotakiwa kuthibitisha baadhi ya taarifa zake binafsi. Taarifa muhimu zinazobebwa na Cheti cha Kuzaliwa ni pamoja na jina la mtoto/mtu, majina ya wazazi wote wawili, mahali alipozaliwa na nyinginezo.
Katika maisha ya kawaida, sehemu nyingi wananchi wamekuwa wakitakiwa kutoa taarifa zilizotajwa hapo juu, lakini siyo kuzitoa tu, bali ni pamoja na kuleta nyaraka ya uthibitisho inayotambulika kisheria ambayo ni Cheti cha Kuzaliwa. Katika mfumo wa elimu nchini Tanzania, mtoto hutakiwa kuanza elimu ya msingi akiwa na umri wa miaka saba na hapa Cheti cha Kuzaliwa huthibitisha umri wa mtoto.
Lakini pia katika huduma za matibabu mzazi anahitajika kuwasilisha vyeti vya kuzaliwa vya watoto wake ili wanufaike na huduma za matibabu kupitia yeye kama mwanachama kwani cheti hutoa utambulisho kwamba waliotajwa ni watoto wake halisi.
Kwa upande mwingine, mwananchi akitaka kupata hati nyingine za utambulisho kama pasi ya kusafiria na kitambulisho cha taifa, Cheti cha Kuzaliwa hutakiwa kama kiambatisho cha msingi kwani uraia na utaifa huanzia katika mahali mtu amezaliwa.
Umuhimu wa Cheti cha Kuzaliwa ni mkubwa na unaendelea kuongezeka. Katika masuala ya kupata mikopo na nafasi za elimu katika vyuo vya elimu ya juu, kupata haki ya kurithi mali kwa mzazi aliyefariki, kumiliki ardhi, na mengine mengi. Manufaa niliyoeleza hapo ni kwa upande wa mwananchi anayepata cheti cha kuzaliwa.
Upo upande wa serikali ambao huhitaji takwimu za wananchi waliosajiliwa kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo na huduma kwa jamii.
Takwimu sahihi na zinazopatikana kwa wakati huiwezesha serikali kutambua kiasi cha ongezeko la wananchi kwa kila eneo na kila wakati kuliko kutegemea takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ambayo hufanyika kila baada ya miaka 10.
Zipo nchi duniani ambazo mifumo yake imetengemaa ambazo watoto wote husajiliwa mara wanapozaliwa na upo mfumo unaosajili watu wote wanaokufa, hivyo ni rahisi kwao kubaini idadi ya wananchi walipo nchini kwa kila wakati. Pamoja na umuhimu wa Cheti cha Kuzaliwa bado wananchi wengi hawana vyeti vya kuzaliwa nchini.
Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 ni asilimia 13.4 tu ndio walio na vyeti vya kuzaliwa na zipo sababu nyingi za kimfumo wa usajili na kihistoria zilizosababisha hali hii.
Changamoto ni kubwa ila kipekee Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) wametambua changamoto hii na kuanza kuifanyia kazi kupitia Mkakati wa Kusajili Matukio Muhimu kwa Binadamu na Takwimu (CRVS) ambao umeanza kutekelezwa kwa sehemu kupitia Mpango wa Kusajili na kutoa vyeti vya Kuzaliwa kwa watoto wa Umri chini ya Miaka Mitano (U5BRP).
Mpango wa Usajili wa Watoto ulianzishwa na RITA na wadau wengine wa usajili kwa lengo la kuhakikisha katika kila eneo ambapo utekelezaji wake umeanza moja, kila mtoto anayeishi na ana umri chini ya miaka mitano anasajiliwa na kupata Cheti cha Kuzaliwa na pili, kila mtoto anayezaliwa katika eneo hilo anasajiliwa na kupata cheti cha kuzaliwa ndani ya muda mfupi baada ya kuzaliwa.
Mpango huu umeleta maboresho makubwa katika mfumo wa usajili kwa watoto kwanza, huduma za usajili wa watoto kusogezwa karibu na maeneo ya wananchi, hivyo huduma kupatikana katika ofisi za watendaji kata na katika vituo vya tiba vinavyotoa huduma za afya ya mama na mtoto.
Umbali kutoka maeneo ya makazi ya wananchi kwenda katika ofisi za wakuu wa wilaya imekuwa moja ya changamoto kubwa iliyosababisha wananchi wengi kutosajiliwa kutokana na gharama zinazoambatana na kufuatilia cheti. Pili, Kuondoa ada ya usajili kwa watoto wa kundi hilo hivyo watoto kupata vyeti bila malipo.
Tatu, Mpango wa Usajili wa Watoto umeongeza uwezo wa RITA kuwa na takwimu kwani simu za kiganjani hutumika katika kuchukua na kutuma taarifa kwenda katika kanzidata ya wakala, hivyo kusaidia utunzaji na upatikanaji wa kumbukumbu.
Kabla ya hapo, ilibidi kusubiri nakala ngumu kusafirishwa kutoka kila wilaya kwenda makao makuu ambapo zimekuwa hazifiki kwa wakati na nyingine kuharibika au kupotea.
Mpaka saa Mpango huu umeanza na unaendelea kutekelezwa katika mikoa 11 ambayo ni Mwanza, Mbeya, Iringa, Songwe, Njombe, Mtwara, Lindi, Geita, Shinyanga, Mara na Simiyu.
Tathmini ya ujumla inaonesha Mpango wa Usajili wa Watoto umefanikiwa sana kwani mpaka kufikia sasa RITA na wadau wengine wamepata mafanikio makubwa katika mpango huu kwani zaidi ya watoto 2,324,349 wamesajiliwa kupitia mpango huu na inategemewa watoto takribani 400,000 zaidi kusajiliwa katika mikoa ya Mara na Simiyu ambapo kampeni ya kuondoa bakaa imezinduliwa wiki hii.
RITA inatekeleza Mkakati huu kwa kushirikiana na wadau wengine ambao ni Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto Duniani (UNICEF), Serikali ya Canada kupitia Shirika Idara ya Mambo ya Nje, Biashara na Maendeleo (DFATD), Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tigo.
Katika mahojiano na Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Emmy Hudson alieleza kwamba mpango wa usajili wa Watoto ni mpango endelevu na siyo kampeni kama ilivyozoeleka na kwamba vituo vinavyosajili kwa sasa ni vya kudumu hata baada ya kumaliza bakaa la watoto wasio na vyeti vya kuzaliwa.
Aliwashukuru wadau wanaoshirikiana na RITA katika utekelezaji wa mpango huu na kuwaomba kushirikiana na Wakala kuwezesha Mpango huu kuenea katika mikoa yote ya Tanzania Bara.
Akielezea changamoto za mpango huu, Hudson alieleza kwamba kumejitokeza taasisi chache ambazo zimekuwa zikivikataa vyeti vinavyotolewa katika mpango huu kwa sababu vimejazwa na mkono na kuhoji mbona taasisi hizo hizo zimekuwa zikivikubali vyeti vya ndoa ambavyo miaka yote vinajazwa kwa mkono.
Alieleza kwamba uhalali wa cheti ni taarifa zilizopo na njia sahihi siyo kuwasumbua wananchi, bali ni kuwasiliana na ofisi ya RITA kwa ajili ya kuvihakiki.
Akielezea kuhusu usajili unaoendelea katika mikoa ya Mara na Simiyu, Meneja Masoko na Mawasiliano wa RITA, Josephat Kimaro alisema kwamba usajili unaendelea vizuri na kwa kipindi cha siku nane tangu kuanza usajili, zaidi ya watoto 277,000 wamesajiliwa katika mikoa hiyo miwili ambayo ni asilimia 37.8 ya lengo.
Mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa na hii inaonesha wananchi wametambua umuhimu wa kuwa na cheti cha kuzaliwa.
Kuhusu mipango ya baadaye kuhusu utekelezaji wa mpango huu, Kimaro alieleza kwamba maandalizi yameshaanza kwa ajili ya kuanza utekelezaji katika mikoa ya Kigoma na Kagera, hivyo kuwataka wananchi kuanza kujiandaa kuwasajili watoto ili wapate vyeti vya kuzaliwa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!