Wednesday 21 February 2018

UGONJWA WA VIDONDA VYA TUMBO NA JINSI YA KUJIKINGA

vidonda vya tumbo 2
Vidonda vya tumbo vinauma sana na humkosesha mgonjwa raha na amani ya maisha. Vinaweza kuwa tumboni au kwenye utumbo mdogo, au kote kwa pamoja! Vinasababishwa na vijidudu aina ya bakteria wajulikanao kama Helicobacter pylori.

Bakteria hao huweza kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine kupitia mate au kula chakula au kunywa maji yenye vijidudu hivyo. Pia dawa jamii ya Asprin huweza kusababisha vidonda vya tumbo endapo mtu atatumia kiasi kikubwa au kwa muda mrefu.
MAMBO YANAYOSABABISHA AU KUONGEZA HATARI YA KUPATA VIDONDA VYA TUMBO
Tumboni kwetu kuna kemikali aina ya asidi ambayo ni kali sana kiasi cha kuweza kutoboa na kuyeyusha hadi vitu vya chuma. Wajua kwa nini kikawaida haitoboi na kuharibu matumbo yetu na utumbo? Kwa sababu tuna utando mzuri sana wa ute tumboni na kwenye utumbo ambao huzuia asidi hiyo isiguse tumbo, utumbo na sehemu zingine za mfumo wa chakula. Tumshukuru sana Mungu!
Vidonda vya tumbo husababishwa, kuchochewa na kuongezwa ukubwa na vitu ambavyo huharibu utando huo au kuzuia uzalishwaji wake hivyo kuacha tumbo na utumbo bila ulinzi dhidi ya asidi kali. Matokeo yake asidi hiyo hugusa tumbo na utumbo na kutoboatoboa sehemu ya juu na kuacha vidonda – vidonda vya tumbo.
Vitu hivyo ni pamoja na
  1. Bakteria aitwaye Helicobacter pylori
  2. Dawa jamii ya Asprin (Kwa mfano Asprin, Diclofenac, Indomethacin na Piroxicam)
  3. Msongo (Stress)
  4. Uvutaji wa sigara
  5. Unywaji wa pombe nyingi                                                                      vidonda vya tumbo 1
Historia ya vidonda vya tumbo katika ukoo wenu na mwili wako kuzalisha asidi nyingi kupita kiasi huweza kukuweka katika hatari ya kupata vidonda vya tumbo pia.
DALILI ZA VIDONDA YA TUMBO
Mara nyingi vidonda vya tumbo huanza polepole na mtu huweza asivigundue hadi pale vinapokuwa vikubwa. Ni vyema kufanya vipimo mara kwa mara na kuwabaini wadudu hawa mapema na kujitibu kabla halijawa tatizo kubwa.
Baada ya vidonda kuwepo kwa muda mtu anaweza kuhisi dalili zifuatazo
  1. Maumivu ya tumbo – Maumivu makali, kuhisi kama unaungua tumboni na kuhisi kama maumivu makali ya njaa
  2. Kupungua hamu ya kula
  3. Kupungua uzito
  4. Kichefuchefu na/au kutapika
  5. Tumbo kujaa gesi
  6. Kutapika matapishi yenye damu
  7. Kujisaidia kinyesi chenye weusi weusi au damu
JINSI YA KUJIKINGA DHIDI YA VIDONDA VYA TUMBO
  1. Hakikisha usafi wa mikono, maji na vyakula mara zote. Zuia Helicobacter pylori asipate nafasi ya kuingia mwilini na kukua hadi kukusababishia vidonda
  2. Epuka kutumia kiasi kikubwa cha dawa jamii ya Asprin kwa muda mrefu
  3. Epuka uvutaji sigara
  4. Epuka unywaji wa pombe nyingi
  5. Epuka mambo yanayoweza kukusababishia msongo na epuka kuwa kwenye hali hiyo
  6. Kula chakula bora na kwa wakati. Epuka kukaa muda mrefu bila kula
  7. Epuka mate kutoka kwa mtu mwingine ambaye hujui hali yake au ana vijidudu vya vidonda vya tumbo
JINSI YA KUDHIBITI VIDONDA VYA TUMBO
Endapo tayari una vidonda vya tumbo unaweza kuvidhibiti vizuri kabisa na visikusumbue tena. Fanya mambo yafuatayo
  1. Zingatia kula chakula bora na ratiba nzuri ya kula, usikae muda mrefu bila kula na usiwe na msongo wa mawazo
  2. Pata matibabu ya kuua hao wadudu jamii ya bakteria wanaosababisha vidonda vya tumbo. Haya ni zaidi ya dawa za kawaida za kupunguza asidi na kutuliza vidonda
  3. Epuka unywaji pombe na uvutaji wa sigara
  4. Epuka vyakula vinavyochochea uzalishwaji wa asidi nyingi tumboni. Mfano ni maharage, kunde, njugu nk
Unaweza ukajikinga dhidi ya vidonda vya tumbo au ukavidhibiti vizuri na visikusumbue tena. Unaweza kuwa na amani na furaha tele maishani mwako bila matatizo ya vidonda vya tumbo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!