Sunday 22 October 2017

Msomi afumbua macho makubaliano na Barrick

MHADHIRI Mwandamizi wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji Semboja amesema hatua ya makubaliano yaliyofi kiwa baina ya serikali ya Tanzania na Barrick Gold Corporation yanaonesha nia njema ya mabadiliko ya utawala unaozingatia matakwa ya wananchi.


Sambamba na hilo, Profesa Semboja amesema ni vyema wananchi wakaelewa kuwa fedha zilizotolewa Dola za Marekani milioni 300 (sawa na Sh bilioni 700), si malipo ya makosa au fidia, bali ni ishara ya kukubali uwepo wa makosa na kuwa yapo makosa yaliyofanywa katika biashara ya madini awali.
Akizungumza na Habari- Leo jana jijini Dar es Salaam, Profesa Semboja alisema hatua iliyofikiwa ni ishara njema ya mabadiliko ya utawala wa serikali ya awamu ya tano, ambayo imeonesha dhamira ya kuzingatia matakwa ya wananchi.
“Kiuchumi haya ni mabadiliko makubwa, sio jambo dogo tulipofika cha msingi sasa ni kuwa makini na mambo tuliyokubaliana ili kuyaweka wazi zaidi kwa sababu hawa wenzetu huwa siku zote wanawaza mbele zaidi,”alisisitiza Profesa Semboja.
Alizungumzia suala la kugawana faida ya asilimia 50 kwa 50, Profesa Semboja alisema ni jambo jema ila linapaswa kufafanuliwa kwani katika masuala ya uchumi kuna faida na hasara, na iwapo kampuni itapata harasa, je, hasara hiyo itagawanywa na serikali.
“Ni vyema ufafanuzi wa hiyo faida ukatolewa kwa sababu katika masuala ya uchumi na biashara kuna faida na hasara na je iwapo kampuni itapata harasa, serikali nayo itahusishwa kushiriki?” Alihoji Profesa Semboja.
Aidha, alishauri kuwa fedha zitakazopatikana katika faida ya biashara hiyo na hizi zitakazotolewa Sh bilioni 700 ni vyema zikaingizwa kwenye akaunti ya Shirika la Taifa la Madini(STAMICO), ili ziboreshe shirika hilo na kutumika kujiendesha kwenye shughuli za madini.
“Ni vyema fedha hizo na zile zitakazokuwa zinapatikana kama faida, zisitumike kwa kazi nyingine bali ziwe zinaingia kwenye mfukowa Stamico ili ipewe nguvu na iweze kujiendesha na kushughulikia masuala yote ya madini, hata ikitokea serikali kwa zile hisa zake 16, ikaambiwa iongeze mtaji, tuwe na fedha na sio kuanza kusuasua wapi pa kuzipata,”alisema Profesa Semboja.
Kuhusu suala la watanzania kuingia kwenye bodi ya menejimenti ya kampuni hiyo, Profesa Semboja alishauri ni vyema kuwa makini katika uteuzi kwani hata awali kwenye kampuni ya Williamson Diamond ambayo nayo ilikufa watanzania walikuwepo na hawakuweza kuisaidia nchi.
Aidha alisema kwenye kipengele cha kampuni za watanzania kupewa kazi za kufanya kwenye migodi hiyo ni vyema nalo likaangaliwa kwa sababu ujanja mwingi hufanyika wa kampuni za kigeni kujisaliji hapa nchini na kuwaingia watanzania wawili au watatu kama wanahisa na hivyo kuhesabika kama kampuni za wazawa jambo ambalo sio sahihi.
“Hili nalo tuwe makini, linafanywa maeneo mengi duniani kumbe ni ndugu au kampuni za wahusika ambazo zimetumia tu mgongo wa kujisajili kwenye nchi husika ili zionekane ni kampuni za wazawa, lakini uhalisia sio kweli ni kampuni za kigeni,’’ alisema Profesa Semboja.
Hata hivyo, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudu aliyeongoza timu ya Tanzania kwenye mazungumzo hayo alifafanua baadhi ya mambo likiwemo suala la faida ya asilimia 50 kwa 50.
Katika ufafanuzi wake alioutoa jana, alisema hiyo asilimia inatolewa baada ya Barrick kulipa kodi zote za serikali na kile kinachobaki baada ya makato ndiyo kinagawanywa nusu kwa nusu. ‘Sasa utaona kuwa serikali sio inapata asilimia 50, bali ni zaidi kama asilimia 70 hivi ya faida, kwa sababu faida inagawanywa baada ya wao kutoa kodi zote za serikali kwa maana nyingine sisi ndio tutafaidi,” alisema Profesa Kabudi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!