Monday 18 September 2017

Madhara ya Sukari mwilini


Related image
Wote tunakubaliana kwamba sukari ni tamu na ni miongoni mwa bidhaa zinazotumika kwa wingi kila siku. Pamoja na umuhimu wake, lakini ni hatari kwa ustawi wa afya pale inapotumiwa kwa wingi kupita kiasi.

Kwa kawaida kiwango cha sukari tunachotakiwa kutumika katika vinywaji vyetu, iwe chai, juisi, na vinginevyo, ni kiasi kidogo sana. Kwa upande mwingine, unapoweka sukari kiasi kidogo, ladha ya kinywaji au chakula hicho huonekana kama haijakamilika.

Katika kutafuta ladha ya sukari iliyokolea, baadhi ya watu hupenda kuweka kiasi kingi cha sukari kwenye vinywaji na vyakula vyao na matokeo yake hujikuta katika matatizo mengine makubwa ya kiafya bila wao kujua kuwa chanzo ni sukari.

Madhara yatokanayo na kupenda sana kula kiasi kikubwa cha sukari ni mengi, baadhi yake ni pamoja na kudhoofika kwa mfumo wa kinga ya mwili (Immunity System), kudhoofika kwa viungo vya mwili, kudhoofika kwa ngozi, kusababisha unene wa kupindukia, n.k.
KIASI KINGI NI KIPI?
Bila shaka unaweza kujiuliza kiasi kingi cha sukari ni kipi? Mazoea yanaonesha kuwa watu wengi huweka sukari kwenye kikombe kimoja cha chai wastani wa vijiko vitatu hadi vinne kama kiwango chao cha kawaida, kiwango ambacho ni kingi mara nne ya kile kinachokubalika.

Wastani unaotakiwa kuwekwa kwenye kikombe kimoja cha chai ni kijiko kidogo kisichozidi kimoja na hata ikiwezekana pungufu ya hapo. Vilevile inashauriwa kujiepusha sana na unywaji wa vinywaji, kama juisi na soda ambavyo huongezewa sukari ya ziada.

Tunaelezwa kwamba chupa moja ya soda huwa na wastani wa vijiko sita vya sukari, kiasi ambacho ni kikubwa kuliko kawaida. Hivyo ni vyema kujiepusha na unywaji wa soda wa kupindukia ukidhani unakunywa kinywaji salama kwa kuwa hakina kilevi.


TUNAWEZA KWELI KUIEPUKA KABISA SUKARI?
Ni dhahiri kwamba hatuwezi kuepuka kabisa matumizi ya sukari na kuiondoa katika milo yetu ya kila siku, lakini uelewa wa madhara yake na dhamira ya kuiepuka inaweza kumsaidia mtu kupunguza kiwango anachotumia kwa siku. Zifuatazo ni baadhi ya dondoo zinazoweza kukusaidia kupunguza matumizi ya sukari:

Anza kuweka mazoea ya kusoma kiasi cha sukari kilichomo kwenye chakula au kinywaji unachokunywa. Mara nyingi kiasi cha sukari kinachowekwa kwenye kinywaji huoneshwa kwa gramu, ambapo kijiko kimoja kidogo cha sukari ni sawa na gramu 4. Hivyo ina maana kwamba iwapo kinywaji au chakula unachokula kina gramu 16 za sukari, hiyo ni sawa na vijiko vidogo vinne.

Kuwa makini na chunguza kwa karibu, kwani vinywaji vingine havioneshi jina la sukari moja kwa moja, badala yake huita kwa majina kama vile ‘high fructose’, ‘molasses’, ‘dextrose’, n.k, hiyo yote ni sukari.
Aidha, ili kupunguza makali ya sukari, kunywa kiasi kingi cha maji kila siku, epuka unywaji wa pombe wa kupindukia na pata muda wa kupumzika au kulala usingizi wa kutosha.
KINGA YA MWILI
Kama tujuavyo, kinga ya mwili ni silaha ya asili ya mwili ya kupambana na maambukizi yoyote yanayosababishwa na bakteria, virusi na parasaiti wengine. Ili kuwa na kinga ya mwili ya uhakika, ni muhimu sana kuimarisha kinga hiyo kwa kula vyakula vyenye virutubisho na kujiepusha na ulaji wa vyakula kama sukari ambayo inaathiri mfumo mzima wa kinga ya mwili.

Kuna ushahidi wa kutosha wa kisayansi kuwa matumizi ya sukari huathiri mfumo wa kinga ya mwili. Seli nyeupe za damu (white blood cells) ndizo seli zinazoimarisha mfumo wa kinga ya mwili, lakini kiasi kikubwa cha sukari kinapoingia kwenye mishipa ya damu, hudhoofisha uwezo wa seli hizo kupambana na bakteria na virusi wanaoweza kuvamia mwili.

Kwa kuzingatia kuwa kinga ya mwili ndiyo msingi wa afya ya binadamu, ni vizuri kujiepusha na matumizi ya vyakula vinavyohatarisha kinga zetu. Lazima ujiulize kama matumizi yako ya sukari ni ya kiwango cha kawaida ama ni ya kuhatarisha afya yako, kama yanahatarisha afya yako, chukua hatua ya kupunguza matumizi yake haraka kabla hujachelewa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!