Tuesday, 8 August 2017

Wakenya kumchagua Rais leo

WAKATI Wakenya wanapiga kura leo ya kumchagua Rais wa nchi, imeelezwa kuwa ukosefu wa ajira, rushwa, gharama za maisha, hali ya usalama na huduma za umma za bure ni miongoni mwa mambo ambayo yanapewa kipaumbele na wapiga kura nchini humo.

Suala la usalama kwa uchaguzi wa leo na baada ya uchaguzi ni jambo linalotazamwa kipekee na Wakenya wenyewe, lakini pia Jumuiya ya Kimataifa hasa kutokana na tukio la hivi karibuni la kutekwa na kuuawa kwa Meneja wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC), Chris Msando.
Pamoja na tukio hilo, wananchi nchini humo wanataka uchaguzi uwe wa amani na haki ili zisijirudie vurugu za mwaka 2007-2008 ambapo watu takriban 1,200 waliuawa baada ya Raila Odinga kupinga ushindi wa Mwai Kibaki. Katika maombi yao kwa taifa juzi kutokana na uchaguzi wa leo, baadhi ya viongozi wa dini walisema walisumbuliwa na kauli za wanasiasa zinazosababisha hofu na wasiwasi kwa wananchi.
“Tuliombea amani na uchaguzi wa haki, tuendelee kutunza amani ili tusije tukaangukia kwenye machafuko kama yaliyotokea mwaka 2007-2008,” alisema Moses Njagi, mmoja wa viongozi wa dini walioendesha maombi ya kuombea amani. Ikumbukwe kuwa Raila Odinga mwenye umri wa miaka 72, anagombea urais wa Kenya kwa mara ya nne; kwa sasa anagombea kwa upande wa upinzani kupitia Muungano wa NASA (National Super Alliance). Kwa Odinga, nafasi hii ni muhimu na huenda ikawa ya mwisho kwake katika kinyang’anyiro cha urais kutokana na umri wake kuwa mkubwa.
Aliwania urais kwa mara ya kwanza mwaka 1997 na baadaye mwaka 2007, 2013 na sasa 2017. Wakati Odinga akigombea urais kwa mara ya nne, Rais Uhuru Kenyatta (56) anatetea nafasi yake ya urais kwa kipindi cha pili kupitia Muungano wa Jubilee. Katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2013, takwimu zinaonesha kuwa Rais Kenyata alimshinda Odinga kwa kupata kura milioni 6.1 wakati Odinga alipata kura milioni 5.3 kati ya kura zote 12.3 zilizopigwa.
Katika uchaguzi wa leo, Wakenya takriban milioni 20 watapiga kura ya kuamua ama kumbakisha Rais Kenyatta Ikulu au kumwingiza Odinga. Kutokana na ushindani mkubwa kati ya wanasiasa hao wawili kwa kipindi chote cha siku 70 za kampeni, Wakenya, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na ulimwengu unasubiri kwa hamu kujua nani ataingia Ikulu ya Nairobi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!