Saturday 29 July 2017

Kuwa muwazi kwa daktari upate tiba yenye uhakika



Kati ya makosa makubwa yanayofanywa na wagonjwa wanapokuwa mbele ya daktari ni kutosema ukweli ili kufanikisha matibabu yao.


Mara nyingi hali hii inasababishwa na aibu.
Mgonjwa anafikiri akisema ukweli wa jambo linalohusu afya yake ataaibika mbele ya daktari anayemuhudumia na mara nyingi hutokea kama daktari na mgonjwa ni jinsi tofauti.

Wengi huwawia vigumu kujieleza hasa matatizo yanayohusiana na afya ya uzazi.
Tofauti ya umri kati ya mtoa huduma na mgonjwa, huweza pia kuwa sababu nyingine ya kuficha ukweli.
Mathalan, inapotokea mgonjwa ana umri sawa au zaidi ya mzazi wa mtoa huduma, huona aibu kutoa siri zake za kiafya kwa mtoa huduma ambaye ni sawa na mtoto wake kiumri.
Usiri huo haumsadii mgonjwa. Kwa faida ya afya yake, anapaswa kuvunja ukimya. Kama kuna sehemu ambayo mtu anapaswa kuwa muwazi kuliko siku zote juu ya mwenendo wa afya yake, basi ni kwenye chumba cha daktari.
Awe daktari wa familia au hospitalini, weka aibu pembeni ukitambua kuwa yupo kwa dhumuni la kukusaidia. Na kadri utakavyompa maelezo ya kutosha, ndivyo unavyomfungulia wigo wa kukutibu kwa uhakika. Mficha uchi hazai, wahenga walisema.
Hivyo basi, kila mmoja anapaswa kufahamu kuwa kuficha tatizo kwa daktari ni hatari hasa tukizingatia ukweli kwamba umuhimu wa tiba unaanzia kwenye maelezo ya mgonjwa kabla hajafanyiwa vipimo.
Zipo taarifa ambazo wengi wamezoea kutosema kwa madaktari ambazo nitazichambua baadhi na kukusihi kuachana nazo kwa sababu madhara yake ni makubwa.
Kunywa pombe
Inapotokea dharura, wagonjwa wengi huwa hawamuelezi daktari kama wamekunywa pombe muda mfupi kabla ya kwenda hospitali ili wasikose matibabu.
Wakati unafikiria kumdanganya, unapaswa kuufahamu ukweli kwamba pombe huchangia kutoa majibu tofauti na tatizo ulilonalo.
Hivyo ni vyema kuwa muwazi kwa sababu itamsaidia daktari kuanza na huduma ya kuondoa kiasi cha pombe kinachozunguka mwilini ili utakapofanyiwa vipimo, upate majibu sahihi yatakayofanikisha matibabu yako.
Kuvuta sigara.
Usidhani ni jambo la kawaida kumficha daktari kama unavuta sigara kwani kuna umuhimu mkubwa yeye kujua ukweli huu.
Baadhi ya tiba hususan ya vidonge hupoteza ubora wake inapokutana na sumu inayopatikana kwenye moshi wa tumbaku ambayo inajulikana kama nicotine.
Kama unavuta sigara, licha ya kumueleza juu ya dalili ulizonazo, ni vema kumwambia daktari ukweli huo.
Kwa kufanya hivyo, utamrahisishia kupangilia tiba ya tatizo lako na kuangalia uwezekano wa kukupangia tiba sahihi na kukusaidia kuacha uvutaji huo kwa kuwa ni hatari kwa afya.
Tendo la ndoa
Inapohitajika tiba ya zinaa, wagonjwa wengi wanakuwa wagumu kueleza ukweli kama wameshiriki tendo hili.
Sababu kubwa hapa ni aibu. Wagonjwa wengi huwa wazito kuwa wawazi kwenye eneo hili na akijitahidi sana basi anaweza kudanganya; ‘nilifanya ngono na mpenzi mmoja tu mwaka huu.’
Nakukumbusha, daktari hayupo kwa ajili ya kukuhukumu ila kukusaidia. Hivyo kuwa muwazi kwa kumueleza idadi halisi ya watu ulioshirikiana nao kwa muda husika, kutamsaidia kukupa huduma unayostahili.
Ugonjwa ya zinaa
Kama una ugonjwa wowote wa wazinaa, unapaswa kukubaliana na ukweli huo.
Kama ulikuwa nao awali, daktari pia anapaswa kujua hilo. Unaweza kuona aibu kulisema hilo lakini unapaswa kujua kuwa baadhi yanaweza kuwa hatari kama hayakupatiwa tiba stahiki.
Ni vema kufahamu kama ulishawahi kuwa na ugonjwa wowote wa zinaa ambao ulitoweka baada ya muda, upo hatarini kujirudia kama haukutibiwa.
Nguvu ya tendo la ndoa
Eneo lingine ambalo wagonjwa huwa wanakuwa wagumu kusema ukweli ni nguvu za jinsi.
Kukosa nguvu za jinsi ni tatizo linaloathiri jinsi zote mbili. Japo imezoeleka wanaume ndiyo wanaopata tatizo la nguvu za kiume, lakini hutokea hata kwa wanawake kukosa za kike.
Hii inaweza kuashiria matatizo mbalimbali ya kiafya kama shinikizo la damu (yaweza kuwa la juu hata la chini), kisukari na magonjwa mengine.
Hivyo, ni vema kumjulisha daktari, kwa kufanya hivyo utamsaidia kukupa tiba ya uhakika.
Najisikia vizuri
Hapa huenda isiwe aibu lakini ni kupuuzia mambo madogomadogo yanayojitokeza kwenye afya ya mgonjwa husika.
Nakukumbusha kutopuuzia dalili zozote zinazojitokeza kwa sababu kupitia hizo, daktari ataweza kubaini matatizo mengine ya kiafya yanayoashiria kujitokeza.
Ni vizuri kuzitilia maanani, mfano maumivu ya kichwa ya mara kwa mara, ya tumbo na viungo au uchovu.
Usipendelee kutumia dawa za kutuliza maumivu mara kwa mara kwa sababu kufanya hivyo huenda kusitatue tatizo, bali unapswa kumueleza.
Dawa za kulevya
Kama ilivyo kwa unywaji wa pombe au uvutaji sigara, dawa za kulevya pia huathiri utendajikazi wa dawa mwilini, hata kuweza kusababisha matatizo makubwa zaidi au hata kifo. Matumizi haya yanaweza pia kusababisha matatizo mengine ambayo daktari anaweza kukuepusha nayo.

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!