Thursday, 29 June 2017

Pacha wa Polisi waangamia ziwani wakisherehekea Idd

WATOTO pacha wa askari polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani kituo cha Bukoba, Koplo Hamisi Kachwamba wamekufa maji katika Ziwa Victoria baada ya mmoja kuzidiwa na maji na mwenzake kujitosa kumwokoa wakati wakisherehekea Sikukuu ya Idd el –Fitr.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi, aliwataja pacha hao kuwa ni Hassan Hamis na Hussein Hamis (12), wanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Kashai, Manispaa ya Bukoba.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi, majira ya saa 11.30 jioni karibu na Hoteli ya Spice, Manispaa ya Bukoba baada ya kuzidiwa na maji wakati wakiongelea katika Ziwa Victoria. Kwa mujibu wa Kamanda Ollomi, pacha hao walikuwa wakisherehekea Sikukuu ya Idd Mosi wakiwa na watoto wenzao.
“Inaelekea mmoja wa pacha hao alizidiwa na nguvu ya maji, pacha mwenzake alijaribu bila mafanikio kumwokoa ndipo naye akazama na kufariki dunia,” alisema. Aidha, alisema kuwa miili ya pacha hao tayari imepatikana na kukabidhiwa kwa familia kwa ajili ya mazishi.
Kamanda Ollomi alisema, “Ni tukio la kusikitisha sana. Ninatoa wito tena kwa wazazi kutowaruhusu watoto wao kwenda kuogelea katika ziwani kama hawana uangalizi wa mtu mzima,” alisema

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!