Saturday 24 June 2017

Bunge lapitisha sheria kupigwa faini ya milioni 1 kwa watakaotupa taka hovyo

No automatic alt text available.

BUNGE limepitisha Muswada wa Sheria ya Fedha kwa mwaka 2017, ambapo pamoja na mambo mengine umeweka adhabu ya kulipa faini ya Sh 200,000 hadi Sh 1,000,000 au kifungo cha mwaka mmoja hadi miwili jela, kwa kosa la kutupa taka ovyo.



Kabla ya muswada huo, faini ya kosa hilo ilikuwa Sh 50,000 na kifungo kisichozidi miezi 12.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Hawa Ghasia, amepinga Serikali kuongeza ushuru kwenye vinywaji baridi, huku kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ikipinga faini za magari barabarani kufanywa sehemu ya mapato ya Serikali.

Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo bungeni jana baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kusoma Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2017, Ghasia alisema kamati yake inaitaka Serikali iangalie upya tozo 14 zilizobakia katika shule binafsi ili nazo ziondolewe kwa lengo la kupunguza gharama uendeshaji kwa shule hizo.

Wakati Ghasia akisema hayo, Naibu Waziri Kivuli wa Wizara ya Fedha, David Silinde, alisema Serikali inatakiwa kuacha tabia ya kugeuza makosa ya barabarani kuwa sehemu ya chanzo cha mapato yake.

Badala yake, alitaka elimu itolewe kwa watumiaji wa vyombo vya moto barabarani ili kupunguza idadi ya makosa hayo.

“Kuna taarifa zisizo rasmi, kuwa maofisa usalama barabarani wamekuwa wakipangiwa idadi ya magari wanayotakiwa kuyakamata kwa ajili ya kukusanya fedha.

“Kutokana na taarifa hizo, askari wa usalama barabarani wamekuwa kero kwa watu kwa sababu wamekuwa wakiwabambikia makosa waendesha vifaa vya moto na kuwafanya waone ni kero kutumia vyombo hivyo,” alisema Silinde.

Katika hatua nyingine, Silinde alisema Serikali ya CCM imekuwa ya kibaguzi na inaonyesha nia mbaya kwa vyama vya upinzani ingawa vimesajiliwa kisheria.

Naye Waziri Mpango, alisema Muswada wa Fedha wa mwaka 2017, umelenga kuzifanyia marekebisho sheria 15 zinazohusu masuala ya fedha, kodi, ushuru, tozo na mawasiliano.

“Marekebisho hayo, yatafanyika kwa lengo la kuweka, kurekebisha, kupunguza au kufuta viwango vya kodi, ushuru, ada na tozo mbalimbali na kuboresha ukusanyaji wa kodi.

“Sheria zilizofanyiwa marekebisho ni Sheria ya Benki Kuu, sura ya 197 ambapo tunataka kuweka sharti la ulazima kwa taasisi za Serikali kufungua akaunti na kuhifadhi mapato na fedha zake Benki Kuu.

“Nyingine ni Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kielektroniki, sura ya 306 ambapo tunalenga kupanua wigo wa mauzo ya hisa za asilimia 25 zitakazouzwa na kampuni ya mawasiliano kwenye soko la hisa kwa kutoa fursa kwa Watanzania, au taasisi yoyote ya kitanzania.

“Fursa hiyo pia itawahusu Watanzania wanaoishi nje ya nchi, kampuni zinazomilikiwa kwa pamoja baina ya Watanzania na raia wa nje, raia na kampuni ama taasisi za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki au raia na makampuni kutoka nchi nyingine.

“Kuondoa sharti la kuuza hisa katika soko la hisa kwa kampuni ndogo za mawasiliano zenye leseni na kubaki na kampuni kubwa zenye leseni ya mtandao au huduma.

“Lengo jingine ni kuwezesha mamlaka ya masoko ya dhamana baada ya kushauriana na waziri mwenye dhamana na masuala ya masoko ya dhamana, kutoa maelekezo ya namna kampuni iliyoundwa kufikia mauzo ya hisa asilimia 25 itakavyoweza kufikia mauzo ya kiwango husika kwa kadri hali ya soko itakavyoruhusu,” alisema Dk. Mpango.

Akizungumzia marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, sura ya 147, alisema kwa kuzingatia mkakati wa Taifa wa kukuza uchumi wa viwanda, kiwango cha ushuru kwa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nchini kimepunguzwa au kubakia ilivyo sasa.

Naye Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alitaka Serikali iweke nguvu zaidi ya kukusanya kodi kwenye michezo ya kubahatisha na kuipeleka kwenye mazingira.

Aliendekeza pia tozo hiyo iongezwe kutoka asilimia sita hadi 12 kwa mapato yatokanayo na michezo hiyo na pia Serikali iongeze tozo hiyo kwenye leseni katika michezo hiyo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema), aliiomba Serikali iondoe Sh 40 kwenye mafuta ya taa kwani kiasi hicho kitaongeza mzigo kwa Watanzania wengi wasio na nishati ya umeme.

Mbunge huyo pia aliitaka Serikali kututumia suala hilo kama njia ya udhibiti na kutaka mfumo ya wa uchakachuaji wa mafuta uimarishwe.

Chanzo: Mtanzania

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!