Tuesday 28 March 2017

Majambazi wafunga barabara ya Kilwa na kupora

MADEREVA saba wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili kisha kuporwa fedha kiasi cha shilingi 920,000 na watu waliofunga barabara ya Kilwa kwa kutumia magogo.


Aidha watu hao licha ya kuwajeruhi na kuwapora fedha pia waliwaibia madereva hao simu saba na kutoweka kusikojulikana.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa kwa vyombo vya habari mjini Kibaha na kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Onesmo Lyanga alisema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 22 majira ya saa saba usiku katika kijiji cha Kitembo kata ya Mchukwi wilaya ya Kibiti.
Kamanda Lyanga alisema kuwa watu hao sita walikuwa na silaha za jadi ikiwa ni pamoja na mapanga na marungu na walizitumia kuwajeruhi madereva hao.
Aidha aliwataja madereva waliojeruhiwa kwa mapanga kuwa ni Issa Juma (26) mkazi wa Jijini Dar es Salaam aliyejeruhiwa shavu la kulia, Badru Uwesu (31) mkazi wa Kisemvule Mkuranga aliyejeruhiwa shavu la kulia na mgongoni, Edward Safari (37) mkazi wa Morogoro.
Aliwataja wengine kuwa ni Ramadhan Ally (34), Nasoro Mohamed (26), Kassimu Omary (36), Khalifa Mohamed wote wakazi wa Mbagala Jijini Dar es Salaam na kuwa majeruhi wote walitibiwa kwenye Hospitali ya Misheni ya Mchukwi na kuruhusiwa kuondoka.
Katika tukio lingine ngombe 102 wamekufa baada ya kunywa maji ambayo yanasadikiwa kuwa hayafai kutumika kwa matumizi yoyote kwenye machimbo ya kokoto.
Kamanda Lyanga alisema kuwa tukio hilo lilitokea Machi 22 mwaka huu majira ya saa 9 alasiri kwenye Kijiji cha Pongwe Msungura Chalinze wilayani Bagamoyo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!