Wednesday 1 February 2017

Wanaochukua sheria mkononi sasa kukiona

SERIKALI itawachukulia hatua watu wote wanaojichukulia sheria mikononi kuwanyanyasa na kuwapiga watu wengine, Imeelezwa.


Akijibu Swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Faida Bakar (CCM), Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alisema, serikali haitasita kumchukulia hatua za sheria mtu anayechukua sheria mikononi kuadhibu watu wengine.
Katika swali lake la nyongeza, Faida alihoji kwa namna gani wanaoharibiwa mazao kama mikarafuu wanalipwa fidia.
Katika swali la msingi, Naibu Waziri Masauni Hamadi Masauni alisema, Jeshi la Polisi nchini linawaonya watu wanaokiuka taratibu, kanuni na sheria za nchi kwa kuwapa vipigo hovyo watu wengine.
Naibu Waziri alikuwa akijibu swali Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema), aliyetaka kujua serikali inachkua hatua gani kulinda wananchi na vitendo vya kikatili, kutokana na vitendo vilivyotokea Sekondari ya Mbeya ambapo walimu walimshambulia mwanafunzi.
Kuhusu suala la walimu waliomshambulia mwanafunzi, Naibu Waziri Masauni alisema suala lipo chini ya Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP) na uchunguzi ukikamilika wahusika watafikishwa mahakamani.
Naibu Waziri alikiri kuwapo kwa vitendo vya kusikitisha nchini na kusema serikali haikubaliani na vitendo hivyo ambavyo ni kinyume cha sheria na utaratibu wa haki za binadamu.
Alisema jeshi la polisi limekuwa likichukua hatua mbalimbali ili kuzuia na kuwalinda raia na mali zao, mara baada ya kupokea taarifa ya matukio mbalimbali na kuyafanyia uchunguzi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!