Sunday 5 February 2017

Balozi Mwinyi awatembelea Watanzania waliofungwa Malawi

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Mzuzu, Malawi. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi amewatembelea Watanzania wanane wanaoshikiliwa katika Gereza Kuu la Mzuzu nchini Malawi.



Watanzania hao, wanane walikamatwa mwishoni mwa Desemba, 2016 kwa tuhuma za kuingia kinyume cha sheria katika mgodi wa urani wa Kayerekera.
Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imesema Balozi Mwinyi alifuatana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Hassan Bendeyeko pamoja na maafisa wengine kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi.
Balozi Mwinyi amewaeleza Watanzania hao kuwa mazungumzo katika ngazi mbalimbali kati ya Tanzania na Malawi yanaendelea na kuna matumaini makubwa kuwa hivi karibuni ufumbuzi wa suala lao unaweza kupatikana.
Alisema yeye na wenzake wamekuja Lilongwe kushiriki kikao cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano (JPCC) kati ya Tanzania na Malawi, lakini wameamua kusafiri takriban kilomita 400 kutoka Lilongwe hadi Mzuzu kuwaona na kuwafikishia ujumbe kuwa Serikali inafanya jitihada kuhakikisha kuwa suala lao linapatiwa ufumbuzi kwa haraka.
"Nikufahamisheni kuwa jitihada katika ngazi mbalimbali kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa tatizo lenu zinaendelea na hata Rais Dk Magufuli alipokutana na Rais wa Malawi, Profesa Peter Mutharika wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika nchini Ethiopia, jambo lenu lilikuwa moja ya masuala waliyoyajadili.
Naibu Katibu Mkuu amesema kuwa alifarijika kuwakuta watu hao wote wapo salama na wenye afya nzuri na kuwajulisha kuwa ziara hiyo ya kuwatembelea na nyingine zilizofanyika siku za nyuma ni ushahidi dhahiri kwao na kwa Watanzania kwa ujumla kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk Magufuli imedhamiria kuwahudumia.
Watanzania hao ambao kati yao wawili ni wanawake wamejitambulisha ni wakulima na wachimbaji wadogo wa madini wanatoka katika mkoa wa Ruvuma walikwenda Malawi chini ya Taasisi ya Caritas kujifunza athari za migodi ya urani katika jamii.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!