Saturday 21 January 2017

Watu 3 huhitaji viungo bandia kila siku MOI

TAASISI ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI), imesema katika idadi yote ya majeruhi wanaowapokea, kila watu 50 wanaofika kunakuwepo na moja ambaye anakuwa ameumia zaidi mguu ama mkono ambao mwishowe inabidi uondolewe.


Katika mahojiano maalumu na taasisi hiyo kuhusiana na suala la kukatwa watu miguu, imeelezwa kuwa ukataji huo wa viungo ni sehemu ya tiba ya katika kuokoa maisha.
Pamoja na kutoa maelezo hayo ya sababu za kukatwa kwa viungo pia taasisi hiyo imesema kwa muda wa mwaka sasa inakabiliwa na changamoto ya kupata viungo bandia vikiwemo miguu na mikono kwa ajili ya kuwawekea watu waliopata ajali mbalimbali, magonjwa ya kansa na kisukari ambayo yamesababisha watu kupoteza viungo vyao.
Changamoto hiyo inatokana na ukweli halisi kuwa kwa siku za hivi karibuni kila siku mtu mmoja, wawili na wakati mwingine watatu hufika katika taasisi hiyo kwa ajili ya kuhitaji viungo bandia.
Sababu ya kiungo kukatwa Mkurugenzi wa Tiba MOI, Dk. Samuel Swai katika mahojiano maalum na gazeti hili jana alisema kama viungo vinakuwa vimeharibika sana husababisha hatari katika maisha ya mhusika na hivyo ni muhimu kukiondoa.
Alisema hayo wakati akifafanua taarifa yake kwamba katika idadi yote ya majeruhi wanaowapokea, kila watu 50 wanaofika kunakuwepo na moja ambaye anakuwa ameumia zaidi mguu ama mkono ambao mwishowe inabidi uondolewe.
“Katika kiungo hicho kinachokuwa kimeumia sana ambacho hakiwezi kubaki, unakuta mishipa ya damu na fahamu imeharibika. Hata kama mguu ama mkono huo utapona hautaweza kutembea. Inatokea na kulazimu kukata viungo hivyo.“
Madai ya bodaboda kukatwa makusudi Alitoa angalizo kuwa kuna dhana potofu iliyojengeka katika jamii kuhusu taasisi hiyo kuwa, wale walioumia na pikipiki wanapofika katika taasisi hiyo wanakatwa mguu hivyo alikanusha hilo na kusema si kweli kwani uamuzi wa kumkata mguu ama mkono mtu yeyote unafanywa na jopo la madaktari wanaokaa na kuona kiungo hicho hakiwezi kutumika tena.
“Tunashauriana na wataalamu wa mishipa ya damu na fahamu kuhusu mguu ama mkono huo, endapo unakuwa umeharibika sana. Hatukati kiungo hicho ovyo ovyo ni lazima mgonjwa ama ndugu aridhie.
“Baada ya kukatwa mguu au mkono, mgonjwa akishapona tunaangalia uwezo wa kutembea au kutumia mkono unafanya kazi namna gani. Kwa kukata mguu kuna uwezekano kabisa ya kumtengenezea mguu wa bandia kiasi akawa anatembea na kuendesha gari. Mguu huo unaweza kuwa mfupi chini ya goti au mrefu juu ya goti,” alisema Dk Swai.
Miguu bandia ya kukimbia Mtaalamu huyo alisema ni maono yao kama taasisi kwa siku za baadaye kuweza kutengeneza mguu au miguu itakayomwezesha mtu anayehitaji kuweza kukimbia.
“Ni miguu miepesi, inatengenezwa kitaalam kabisa hapa kwetu hatujafikia utaalamu huo,” alisema. Alieleza changamoto kubwa wanayokutana nayo ni kuagizwa kwa vifaa hivyo nje ya nchi ambavyo ni ghali.
Kwa maelezo ya Dk Swai, miguu mizuri inayoagizwa nje gharama yake inakuwa kubwa kiasi kwamba mtu wa kawaida hawezi kuimudu.
Gharama ya mguu bandia chini ya goti ni Sh 600,000 na juu ya goti ni Sh milioni 1.5.
Kwa upande wa mikono juu ya kiwiko ni Sh. milioni 2.5 na chini ya kiwiko ni Sh milioni 1.5. Akizungumzia utengenezaji wa viungo hivyo bandia iwe ni mguu au mkono alisema kuwa vinachukua muda wa kama mwezi mzima hadi miezi miwili kwani mchakato wake ni mrefu.
Alisema kama taasisi wamejitahidi kuzungumza na Mifuko ya Bima ili waweze kuweka gharama hizo za viungo kwa kuwa zipo juu.
Akizungumzia majeruhi anayetaka kuvaa kiungo bandia alisema inategemeana na alivyoumia kwani hupona ndani ya miezi mitatu hadi sita.
Akizungumzia suala la ukataji wa viungo katika taasisi hiyo, alisema ndani ya miezi mitatu anakuwepo mtu wa kukatwa kiungo, lakini mara nyingine kwa mwezi moja hukatwa wawili au watatu inategemeana. Kushamiri kwa imani za kishirikina
Ametoa angalizo kuwa kutokana na mila za kiafrika watu wengi wanakuwa na uoga mkubwa wa kukata kiungo chochote, na kwamba imeshafikia wakati mgonjwa anakaribia kufa kutokana na sumu anayopata kutokana na kuharibika kwa kiungo, ndugu wanakuwa wanakataa kabisa asikatwe.
“Ndugu wengine wanasema kuliko mgonjwa akatwe kiungo chake ni bora waondoke naye,” alisema na kuongeza kuwa katika hilo elimu inahitajika jamii kulikubali suala hilo.
Alisema kauli mbiu yao ni kuhakikisha wanaponyesha maisha ya mgonjwa na kuokoa kiungo cha binadamu kisikatwe, na kiokolewe kiungo ambacho kikibakizwa kinaweza kufanya kazi, hivyo hatua ya kukata kiungo inakuja mwisho baada ya jitihada zote kushindikana.
Alisema kwa watoto wanaowekewa viungo kwa kuwa wanaendelea kukua inabidi kila baada ya miezi sita kurudi hospitali na kutengenezewa tena.
Mtaalamu wa viungo bandia katika taasisi hiyo, Charles Mahua alisema kwa mwaka wanapokea zaidi ya watu 100 wanaohitaji viungo bandia, kwani kila siku amekuwa akishuhudia mtu mmoja hadi watatu wanafika kwa ajili ya huduma hiyo.
“Hivi sasa kuna kesi za ajali za barabarani, ugonjwa wa kisukari na kansa ambazo zote hizo zinasababisha watu kupoteza viungo,” alisema Mahua.
Alisisitiza kuwa ukosefu wa vifaa endelevu ndio changamoto kubwa katika taasisi hiyo kwa kuwa wanaweza kupata vifaa halafu vinaisha.
Alisema zaidi ya mwaka walikuwa hawana vifaa, lakini miezi miwili iliyopita walipata miguu 400 bado wanahitaji mikono. Alisema wananchi wengi hawana uwezo wa kulipia gharama halisi, na kwamba kwa sasa bima ya afya huwa hailipi katika eneo hilo.
Alisema changamoyo nyingine ni upungufu wa wafanyakazi kwani kama wangekuwa na vifaa vyote, watumishi wa afya wa kutoa huduma pia wasingetosha.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!