Friday 11 November 2016

Rais alia akimuaga Mungai

RAIS John Magufuli amebubujikwa na machozi hadharani wakati akiongoza mamia ya waombolezaji jijini Dar es Salaam, kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri katika awamu nne za uongozi wa nchi na Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, Joseph Mungai, aliyefariki ghafla Novemba 8, mwaka huu.


Mbali na Dk Magufuli, Rais mstaafu Benjamin Mkapa, mke wa Rais mstaafu Mama Salma Kikwete, Makamu wa Rais wa Awamu ya Nne, Dk Mohamed Gharib Bilal, mawaziri wakuu wastaafu Jaji Joseph Warioba na Frederick Sumaye, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Damian Lubuva, mawaziri na viongozi wengine mbalimbali walitoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Mungai, katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam jana.
Baada ya shughuli hiyo, mwili wa Mungai ulipelekwa nyumbani kwake Osterbay kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa kwa maziko, yatakayofanyika kesho.
Kabla ya kutoa heshima za mwisho, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga, alimwelezea Mungai kuwa alikuwa na kipaji cha tofauti cha uongozi tangu akiwa mdogo.
“Uongozi pekee ni tunu. Mungai alikuwa na sifa ya uongozi. Lakini kipindi cha uongozi ni jinsi unavyotafsiri uongozi wako kwa wale unaowaongoza. Alitumia kipaji chake cha uongozi kwa jamii,” alisema Balozi Mahiga na kubainisha kuwa baba mzazi wa marehemu alitokea Kenya na mama yake mzazi alitoka katika ukoo wa Chifu Mkwawa.
Naye mtoto wa marehemu, Jim Mungai, alisema baba yake alikuwa Mbunge kwa miaka 35 katika Jimbo la Mufindi na baadaye baada ya kugawanywa Mufindi Kaskazini.
Alisema katika miaka yake hiyo kwa awamu nne alikuwa Waziri wa Kilimo, Elimu, Mambo ya Ndani, Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM. Alisema ameacha mke na watoto saba.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu Sumaye alimwelezea Mungai na kusema kuwa katika kipindi chake cha uwaziri, alikuwa waziri wa elimu mchapakazi, mwadilifu na kwamba aliongoza wizara hiyo vizuri hadi viwango vya elimu viliongezeka.
“Tumempoteza mtu muhimu sana katika nchi,” alisema Sumaye.
Aliyekuwa Waziri katika Awamu ya Nne, Steven Wassira alisema alifanya kazi na Mungai katika wizara moja ya kilimo, akiwa Naibu Waziri wake wa Kilimo.
Aliongeza kuwa Mungai alipenda kuona mabadiliko ya kilimo katika sekta zote ndio maana karibu awamu zote nne aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo.
Mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale-Mwiru alimwelezea Mungai kuwa alikuwa mtu aliyekuwa na kichwa kizuri katika utendaji kwa kuwa katika nafasi zote alizopewa alikuwa mchapakazi.
“Alikuwa akitoa mchango bungeni alioufanyia utafiti wa kina na unakuwa ni wa kujenga,” alisema. Serikali imemteua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuiwakilisha kwenye maziko yatakayofanyika kesho.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!