Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Paul Makonda akizungumza na wananchi waliojitokeza katika viwanja vya mnazi mmoja kupima afya bure.


JESHI la Polisi jana lililazimika kuongeza nguvu katika viwanja vya Mnazi Mmoja kulinda maelfu ya wananchi waliofurika kwa ajili ya kupima afya zao.
 


Wananchi hao walianza kumiminika uwanjani hapo kuanzia saa 10 alfajiri huku wengine wakibeba vyeti mbalimbali vya hospitali kwa lengo la kuchangamkia fursa ya kukutana na madaktari bingwa, ambao walikuwa wakitoa huduma za vipimo na ushauri.
Upimaji huo wa afya uliandaliwa na kuratibiwa na Dar Afyacheck kwa lengo la kuwafikia watu 50,000 ambao watapimwa na kupata ushauri.
Nipashe ilishuhudia majira ya saa sita mchana, jeshi la polisi likiongeza idadi ya askari baada ya utaratibu ambao ulipangwa na waandaaji kuvurugwa na wananchi na kusababisha baadhi ya madaktari hadi muda huo, kushindwa kuwaona mgonjwa.
Katika hali isiyo ya kawaida, baadhi ya watu walifika eneo hilo na kuwahi namba za mwanzo ambao walikuwa wakiziuza kitendo ambacho kilisababisha kitangazwe hadharani ili watu waiingie mkenge.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Uhuru ya jijini Mwanza, Dk. Derick Nyasebwa, ambaye ni daktari wa magonjwa ya moyo, alisema wananchi wameshindwa kufuata utaratibu na kusababisha kukwama kwenye eneo moja la kuingiza taarifa kwenye mfumo wa kompyuta.
"Hadi sasa sijaona mgonjwa hata mmoja kutokana na utaratibu kutofuatwa na wananchi," alisema.
Aidha, alisema lengo la huduma hiyo ni kuipatia serikali takwimu sahihi za magonjwa na kwamba imepangwa kufanyika siku hiyo tu.

"Takwimu zilizopo serikalini zinawahusu wagonjwa ambao wanafika kwenye vituo vya afya wakiwa tayari kwenye hatua ya kuumwa, wengine magonjwa yakiwa katika hatua ambazo sio za kuridhisha, lakini leo takwimu zitakazokusanywa hapa nyingi ni za watu ambao wapo katika hatua ya awali ya ugonjwa," alisema.
Alisema uwepo wa takwimu zisizo sahihi kama ambapo idadi ya wanaoumwa imechangia serikali wakati mwingine kuingiza dawa, chanjo pungufu.
"Umewahi kujiuliza kwa nini chanjo zinakuwa adimu, sababu ni takwimu zinazokusanywa ama haziwafikii wahitaji mwisho wa siku serikali inazitumia kuagiza chanjo ambazo zinakuwa pungufu kama hivi sasa hakuna chanjo," alisema.
Naye Mratibu wa Dar Afyacheck, Dk. Isaac Maro, alisema lengo lao ni kuifikia idadi hiyo ya watu na kwamba hadi saa nne asubuhi jana walikuwa tayari wametoa namba zaidi ya 1,000.

Alisema umati uliojitokeza siku hiyo ni kiashiria kwa serikali kuwa watu wanaumwa lakini hawana fedha.
"Serikali katika mipango yake iangalie kwa namna ambavyo kila Mtanzania anapata kadi ya bima, unakuta mtu anaumwa lakini kutokana na kukosa fedha anameza panadol maisha yanaendelea na siku ambayo analetwa hospitali anakuwa kwenye hatua ya mwisho ya ugonjwa,” alisema.

Abuu Peter, mkazi wa Ilala aliyekutwa kiwanjani hapo, alisema kupima ni jambo la msingi kwa sababu wakati anakwenda hapo akijua anaumwa kutokana na maumivu anayosikia lakini baada ya vipimo amekutwa hana tatizo.

NIPASHE.