Tuesday 27 September 2016

Rais magufuli kuzindua ndege mbili za ATC kesho


Na Lilian Lundo-MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli anatarajiwa kuzindua ndege mbili za Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) zilizonunuliwa kwa kutumia kodi za wananchi.

Uzinduzi huo unatarajiwa kufanyika kesho Septemba, 28 mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 1).

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu (Uchukuzi), Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Leonard Chamuriho leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa ndege hizo.

Dkt. Chamuriho alisema kuwa ndege ya kwanza iliwasili nchini tarehe 20/09/2016 na ndege ya pili inatarajiwa kuwasili nchini leo tarehe 27/09/2016 kuanzia saa 6:00 mchana.

Vile vile Katibu Mkuu huyo alisema kuwa ndege hizo zimenunuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuhudumia wananchi wa ndani ya nchiya Tanzania na nchi jirani.

“Ndege hizo aina ya Dash 8 Q400 zimetengenezwa na kiwanda cha Bombadier nchini Canada ambapo kila moja ina uwezo wa kubeba abiria 76 na zitatumika katika kuhudumia soko la ndaniya Tanzania na nchi jirani,” alifafanua Dkt. Chamuriho.

Aidha, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inawakaribisha wananchi wote kushuhudia uzinduzi wa ndege hizo unaotarajiwa kuanza saa mbili kamili (2:00) asubuhi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!