Tuesday 27 September 2016

Mtoto aishi miaka 15 bila sehemu ya haja kubwa

MTOTO Flora William wa kijiji cha Mandi wilayani Babati, Manyara aliyezaliwa akiwa na ulemavu wa kutokuwa na sehemu ya haja kubwa, ameendelea kuteseka kwa miaka 15 sasa kutokana na wazazi wake kutokuwa na uwezo wa kuwezesha matibabu yake.


Licha ya kuteseka, amekuwa na wakati mgumu kutokana na kunyanyapaliwa na watoto wenzake, sababu kubwa ikielezwa ni kutumia sehemu ya tumbo kutoa haja kubwa.
Wazazi wa mtoto huyo, Stella Martin ambaye ni mama na mumewe William Philipo, wamezungumzia hali hiyo inayomkabili mtoto wao.
Stella, alisema alimzaa akiwa na hali hiyo na alipojaribu kumweleza mama mkwe wake alimtaka asimwambie mtu yeyote, akidaiwa kusema itakuwa aibu kuieleza jamii inayowazunguka kuwa mtoto huyo hana sehemu za haja kubwa.
Alisema alijaribu kumsihi mume wake kumpeleka mtoto huyo hospitali akiwa bado mdogo ili atibiwe na kubahatika kwenda katika Hospitali ya Hai mkoani Manyara alikopata matibabu ya kupasuliwa sehemu za mbavu.
Alisema baadaye waliambiwa wampeleke mtoto huyo katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC iliyopo Moshi, mkoani Kilimanjaro kwa matibabu zaidi ambako walitakiwa kugharimia Sh 200,000 ili mtoto aweze kutibiwa, lakini hawakuwa na fedha hizo.
Kutokana na hali hiyo, mama huyo alisema walilazimisha kurejea nyumbani ili kutafuta fedha zaidi, lakini hawakufanikiwa na hivyo kuendelea kubaki na mtoto wao ambaye kwa sasa amekua na kufikisha umri wa miaka 15.
Inaelezwa kuwa, hali ya mtoto huyo kadri anavyozidi kukua inazidi kuwa mbaya kutokana na sehemu alizopasuliwa kwa ajili ya kutolea haja kubwa tumboni kwake. Kwa mujibu wa mama wa mtoto huyo, kwa sasa utumbo umetoka nje hivyo inamlazimu kujifunga tumboni mfuko mweusi wa Plastiki wakati wa kujisaidia ili kuhifadhi kinyesi chake.
Baba mzazi wa mtoto huyo, alisema kwa sasa hana fedha za kumpeleka mtoto huyo hospitali kutokana na kuwa na hali duni ya uchumi, hivyo kuwaomba Watanzania wajitokeze kumsaidia aweze kumpeleka mwanawe huyo hospitali.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!