Friday 26 August 2016

SIMANZI


  • Vilio, huzuni vyatawala polisi waliouawa wakiagwa Dar, msako mkali wa kukamata wauaji waendelea..
SIMANZI, vilio na majonzi vilitawala jana wakati majeneza yaliyohifadhi miili ya askari polisi watatu kati ya wanne waliouawa jijini Dar es Salaam yalipofikishwa kwenye viwanja vya Polisi Barracks jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho.



Baadhi ya askari na raia waliohudhuria tukio la kuuagwa miili ya askari watatu kati ya wanne waliouawa kwa risasi na majambazi.

 

Usiku wa kuamkia juzi, askari wanne wa jeshi hilo waliuawa kwa kupigwa risasi na raia wawili kujeruhiwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakati wakibadilishana lindo kwenye eneo la tawi la benki ya CRDB Mbande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Askari waliouawa ni Koplo Yahya Malima, Konstebo Tito Mapunda, Konstebo Gaston Lupanga na Koplo Khatibu, ambaye mwili haukuwapo kwenye shughuli hiyo kutokana na kuchukuliwa mapema na familia yake.
Mamia ya watu wakiwamo askari na wanafamilia walioongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, walipatwa na hali hiyo baada ya magari matatu kuwasili kila moja likiwa na jeneza lake huku kukiwa na ulinzi mkali eneo hilo.
Waombolezaji walianza kuwasili kuanzia saa 4:00 asubuhi kwa ajili ya kuaga miili hiyo ya askari hao huku viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwamo Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Ernest Mangu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda nao wakishiriki.
Wengine waliofika kwenye shughuli hiyo ni pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Diwani Athumani na maofisa wengine wa juu wa Jeshi la Polisi.
WAZIRI ALONGA
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Nchemba, alisema wataweka utaratibu wa bima za maisha kwa watumishi wote wa jeshi hilo ili wanapopoteza maisha, familia zisiachwe zikiwa na shida.

Nchemba alisema kuwa kwa sasa hakuna utaratibu maalum wa kusaidia familia hizo na hasa katika masuala ya ujenzi wa nyumba.
Alisema uongozi wa wizara utakaa na kuangalia jinsi ya kusaidia familia za waliofariki katika tukio hilo wakati mchakato wa kuanzishwa bima ukiandaliwa.
Kiongozi huyo wa serikali aliwataka askari kuwa makini kwa kuwa sasa wamekuwa wakilengwa na kwamba tukio la usiku wa kuamkia juzi lisiwe chanzo cha woga na kuwavunja moyo, bali liwape ujasiri wa kupambana na uhalifu.
IGP MANGU AONYA
IGP Mangu alisema Rais John Magufuli ametoa pole kwa wafiwa na ndugu jamaa na marafiki na kuahidi kupatia kila familia rambirambi ya Sh. milioni 10.

Aliendelea kueleza kuwa jeshi hilo lina utaratibu wa kutoa kifuta machozi cha Sh. milioni 15 kwa familia na taratibu za wanafamilia kupata rambirambi hizo zitafanyika baada ya vikao vya familia kutoa uamuzi.
IGP Mangu aliendelea kueleza kuwa watawashughulikia wale wote walioonyesha kufurahishwa na mauaji hayo wakiwamo wale ambao wametamka hadharani kuwa watapambana na jeshi hilo.
Alisema kuna watu ambao wamekuwa wakitoa taarifa kwenye mitandao na kuonyesha kufurahishwa na mauaji hayo, hivyo watatiwa nguvuni ili wafafanue kufurahishwa kwao kuna uhusiano gani na waliotenda uovu huo.
SIRRO ATANGAZA 'VITA'
Kwa upande wake, Kamanda Sirro alisema kitendo cha kuwavizia na kuwaua askari polisi hao ni sawa na kuwasha moto.

“Hawa wamewasha moto, sisi tutaukoleza na watakiona. Tutajibu mapigo na tutapiga kwelikweli,” alisema Kamanda Sirro.
Alisema jeshi lake linafanya jitihada za kuwasaka wahalifu ili wachukuliwe hatua huku akiwataka askari kuhakikisha wanawapata wahalifu hao.
MAKONDA ALIA
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda alisema unyama uliofanywa na watu hao ambao bado wanatafutwa ni wa kutisha huku akiliagiza Jeshi la Polisi kuwashughulikia watu wanaohisi wana nia mbaya.

“Hakuna kitu kinachouma kama kupata taarifa za kifo cha mtu unayemthamini. Nikiwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa, nakuagiza Kamanda wangu Sirro mkiwapata watu wenye nia kama hizo msiwaache hata watu wa haki za binadamu waseme,” alisema.
Makonda alisema kumekuwa na watu ambao wanadai kutetea haki za binadamu, lakini ili wathibitishe kuwa wanatetea kweli wangeandamana kupinga mauaji ya askari hao ambao walikuwa wakilitumikia taifa.
Aliomba Wizara ya Mambo ya Ndani kufikiria kusaidia familia za marehemu hao kwa kuwapatia nyumba ili ziwasaidie baada ya kuondokewa na wapendwa wao.
Alisema katika kupambana na hali hiyo, polisi wasiogope watu wa haki za binadamu wanapofanya uamuzi.
"Kama wanataka kulalamikia haki za binadamu, basi waje kwangu," alisema Makonda huku akikatisha salama zake baada ya kushindwa kujizuia kububujikwa na machozi.
KAULI YA TUME YA HAKI
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Bahame Tom Nyanduga, alisema wanalaani na kupinga mauaji hayo na kuwataka wananchi kuzingatia haki na utawala bora.

"Tutaendelea kutetea haki ya kuishi ya kila Mtanzania, tume imeundwa kikatiba, hivyo kila mtu anastahili haki hizo."
ASKARI WALIOUAWA
Koplo Yahya alizaliwa kijiji cha Kibuta wilayani Kisarawe mwaka 1966 na alijiunga na jeshi hilo mwaka 1992 kabla ya kupandishwa cheo cha koplo mwaka 2011. Ameacha mke na watoto watatu.

Konstebo Tito alizaliwa kijiji cha Migoli mkoani Iringa mwaka 1990 na baada ya kuhitimu elimu ya sekondari, akajiunga na jeshi hilo hadi kifo kilipomkuta akiwa kazini.
Konstebo Gaston alizaliwa mwaka 1987 mjini Songea mkoani Ruvuma na baada ya kuhitimu kidato cha nne, alijiunga na jeshi hilo mwaka 2011.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!