Tuesday 9 February 2016

JARIDA LA WANAWAKE-JINSI YA KUZUIA MIMBA

Katika kipindi chote cha maisha yake, mwanamke hutoa mayai ya uzazi zaidi ya 400. Hutoa yai moja kwa kila mwezi kwa wastani wa miaka 30.
 Yai hili linapokutana na mbegu ya kiume wakati au baada ya kufanya ngono, linaweza kurutubishwa na mimba ikatungwa.


Ili kuzuia mimba isitungwe, kuna njia za uzazi kuzuia mimba au zikijulikana pia kama njia za uzazi wa mpango. Njia hizi za kuzuia mimba huzuia yai la mwanamke kukutana  na mbegu za kiume.
Katika kuchagua njia ya kuzuia mimba ni muihimu kuzingatia;
·         Ufanisi wa ufanyaji kazi wa njia hiyo.
·         Inafanya kazi kwa muda gani (ukizingatia unataka kukaa bila kupata mimba kwa muda gani).
·         Madhara ya utumiaji wa njia hiyo.
·         Kama inaweza kuachwa na wewe kupata ujauzito mapema (kuna njia ambazo  huchelewesha kidogo kupata ujauzito baada ya kuziacha).
·         Kama itakulinda dhidi ya magonjwa ya zinaa.
Kuna makundi ya aina mbili ya njia za kuzuia mimba;
·         Njia za homoni
·         Njia zisizo za homoni
Njia za Homoni
Njia za homoni ni njia ambazo zimekuwa zikitumika muda mrefu kuzuia mimba na zenye ufanisi mkubwa sana. Hutumia homoni za kutengenezwa (progestin na oestrogen) ambazo huzuia mayai ya kike yasitoke kwenye ovari.  
Homoni hizi hufanana na zile zinazotengenezwa mwilini. Ovari huendelea kutoa mayai pale ambapo mwanamke anaacha kutumia njia hizi. Njia hizi huweza kuwa na homoni ya progestin peke yake au mchanganyiko wa progestin na oestrogen.
Namna Zinavyofanya Kazi
Homoni hizi hufanana na zile zinazotengenezwa na mwili kwa kawaida. Huzuia mimba kwa kuongezeka kwenye damu kwa kipindi tofauti na;
·         kuzuia ovari zisitoe mayai ya uzazi.
·         kuufanya ute kwenye shingo ya uzazi kuwa mzito na mgegu za kiume kushindwa kupita.
·         kuufanya mji wa uzazi usiwe tayari kupokea kiinitete.
Njia hizi ni;
Vidonge Vya Kuzuia Mimba
Hujulikana kama oral contraceptives  kwa kingereza na kuna vya aina mbili, vyenye progestin na oestrogen (combined oral contraceptive) na zenye progestin peke yake (progestin only contraceptive).
Mwanamke hunywa kidonge kimoja kila siku na vina ufanisi mkubwa katika kuzuia mimba.
Sindano za Kuzuia Mimba.
Hujulikana kama injectable contraceptives kwa kiingereza. Huwa zina homoni ya progestin ambayo huchomwa kila baada ya wiki 12. Zina ufanisi mkubwa na hufanya kazi kwa muda mrefu.
Vitanzi.
Vikijulikana kama  intrauterine contraceptive devices  kwa kiingereza, hupandikizwa kwenye mji wa uzazi na huwa na homoni yaprogestin. Hufanya kazi kwa muda mrefu na kwa wastani wa miaka minne.
Vipandikizi
Vijiti huitwa implants kwa kiingereza.  Mara nyingi hupandikizwa kwenye mkono na huwa na homoni ya progestin ambayo huingiapolepole kwenye damu kwa muda mrefu.
Hufanya kazi kwa wastani wa miaka 4, ingawa kuna vingine vikiwa na muda mrefu zaidi. Huweza kutolewa pale mwanamke anapoamua.
Ufanisi
Njia hizi za homoni zina ufanisi mkubwa, zikiwa na uwezo wa kuzuia ujauzito kwa zaidi ya asilimia 99.
Wanawake wasioshauriwa kutumia njia za homoni;
·         Mwanamke mwenye historia ya saratani ya matiti.
·         Mwanamke mwenye shinikizo la damu la kupanda.
·         Mwanamke mwenye ugonjwa wa moyo.
·         Mwanamke mwenye matatizo ya damu kuganda kwenye mishipa (deep venous thrombosis).
·         Amefanyiwa upasuaji ambao utasababisha asitembee kwa muda mrefu.
Faida ya Njia za Homoni
Utumiaji wa njia za homoni huwa na faida nyingi, hasa zifuatazo;
·         Hupunguza hatari ya saratani za uzazi, ovari na utumbo.
·         Hupunguza maumivu ya tumbo wakati wa hedhi.
·         Hupunguza kiasi cha damu inayotoka wakati wa hedhi.
·         Ni rahisi kutumia na zina ufanisi mkubwa.
Madhara ya Njia za Homoni
Utumiaji wa njia hizi huweza kuleta madhara pia, hasa zinapotumika kwa muda mrefu sana. Ingawa sio lazima madhara yampate kila  mtumiaji, madhara haya yanaweza kuwa;
·         Hatari ya kupata saratani ya titi huongezeka.
·         Kulainika mifupa.
·         Damu kuganda kwenye mishipa.
·         Kiharusi (stroke).
Njia Zisizo za Homoni
Njia hizi huzuia mbegu za kiume zisikutane na yai la mwanamke. Zipo za aina mbalimbali, nyingine zikihusisha upasuaji mdogo na mkubwa. Njia hizi hujumuisha;
Kondomu
Hii ni njia maarufu sana, huzuia mbegu za kiume zisifikie yai la uzazi. Kuna kondomu za kike na kiume, zote zikiweza kufanikisha hili.
Pia hukinga dhidi ya VVU na magonjwa ya zinaa.
Njia za asili
Njia za kalenda, ute wa kwenye uke na joto hutumika kuzitambua siku za hatari na hivyo kukwepa ngono katika kipidi hicho. Pia kumwaga nje ni njia nyigine katika kundi hili.
Kufunga mirija ya mayai (tubal ligation).
Upasuaji hufanyika na mirija ya mayai hufungwa na kuzuia mbegu zisifikie mayai ya uzazi. Njia hii ikitumika mwanamke hataweza kuzaa tena kwa kawaida.
Kufunga mirija ya manii (vasectomy).
Upasuaji mdogo hudfanyika na mirija ya kupitisha mbegu kutoka kwenye koroodani hufungwa. Hivyo mwanaume hutoa shahawa zisizo na mbegu. Mirija ikifungwa mwanaume hawezi kuvaa tena.
Vitanzi
Hivi hupandikizwa ndani ya tumbo la uzazi, huwa vimetengezwa kwa kutumia madini ya shaba ambayo huzuia mimba kutungwa .
Huweza kutumika mpaka miaka 4. Tofauti na vitanzi vinavyotumika kwenye njia za homoni, vitanzi huwa na madini ya shaba.

Njia hizi zisizo za homoni zina ufanisi kwa viwango tofauti, kuna ambazo zina ufanisi mkubwa na zile zenye ufanisi mdogo kama njia za asili. Kuna ambazo zinaweza kuleta madhara na nyingine ambazo haziwezi kuleta madhara.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!