Monday 30 November 2015

WATAKAOSHINDWA KUPELEKA WATOTO SHULE KUKIONA!


SERIKALI imeonya kuwa itawachukulia hatua za kisheria wazazi na walezi watakaoshindwa kuwapeleka watoto shule na kusisitiza kila mtoto anapaswa kupewa haki ya kupata elimu itakayoanza kutolewa bure kuanzia Januari.


Sera ya utoaji wa elimu bure ni moja ya vipaumbele vilivyowekwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ili kuhakikisha mtoto wa kike na wa kiume nchini kote anapata elimu bila kuwepo kwa kisingizio.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju alitoa onyo hilo jijini Dar es Salaam wakati akihutubia kwenye Mahafali ya Shule za Kimataifa za Feza mwishoni mwa wiki.
Alisisitiza hatua za kisheria zitachukuliwa bila kuwepo kwa huruma dhidi ya wazazi au walezi watakaotaka kurudisha nyuma jitihada za Rais za kutaka kuwa na Taifa la watu walioelimika.
“Kumfanya mtoto kuacha shule kwa sababu yoyote ile ni kosa la jinai kwa vile kunamkosesha haki yake ya msingi ya kupata elimu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mikataba mingine ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia,” alifafanua Masaju.
Alikwenda mbali zaidi kwa kusema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kutoa elimu bora na kwa usawa kwa watu wote ili kukabiliana na ujinga ambao ni moja ya maadui wa taifa kama ilivyosisitizwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
“Serikali mara zote imekuwa ikiwekeza kwenye elimu na kuwahamasisha wadau wengine wakiwemo washirika wa maendeleo kuwekeza katika elimu, kama walivyofanya wamiliki wa Shule za Feza, lengo likiwa ni kusaidia upatikanaji wa elimu bora kama inavyosisitizwa na serikali mara zote,” alisema Masaju.
Masaju hakusita kuipongeza Menejimenti ya Shule za Feza kwa kutoa uhuru wa kuabudu kwa wanafunzi wa shule hizo na kutoa mwito kwa viongozi wa shule za serikali na za binafsi kuzingatia haki hiyo kama inavyosisitizwa kwenye Katiba na kwamba Serikali itachukua hatua kali za kisheria kwa watakaopuuza utoaji wa haki hiyo.
Awali, Menejimenti ya Feza iliiomba Serikali kuingiza masuala ya maadili na imani katika mfumo wa elimu wakisema ndiyo yamekuwa yakiongeza chachu ya kuwafanya wanafunzi wa shule hiyo kufanya vizuri kielimu kila mwaka.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!