Thursday 3 September 2015

MVUA KUBWA ZINATARAJIWA KUNYESHA



Maeneo mengi nchini yanatarajiwa kupata mvua kubwa katika kipindi cha mvua za vuli zinazotarajiwa kuanza kunyesha wiki hii na kusababisha maafa katika maadhi ya mikoa.


Mvua hizo ambazo zimeelezwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) kuwa ni za juu ya wastani zitanyesha zaidi katika mikoa ambayo ina kawaida ya kupata mvua mara mbili kwa mwaka.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi (pichani), wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kutoa utabiri wa mvua kwa kipindi cha miezi mitatu ya Oktoba, Novemba na Desemba, mwaka huu.
“Katika kipindi hiki cha mvua kubwa kutakuwa na athari mbalimbali ikiwamo mlipuko wa magonjwa na uharibifu wa miundombinu,” alisema.
 Dk. Kijazi alisema maeneo ya Kanda ya Ziwa (Kagera, Mwanza, Geita, Simiyu, Mara na Shinyanga), inatarajiwa kuwa na mvua kubwa zitakazoanza kunyesha wiki ya tatu ya mwezi huu kuanzia Septemba 22.
Alisema mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara nayo inatarajiwa kuwa na mvua kubwa kuanzia wiki ya kwanza ya mwezi ujao.
Dk. Kijazi, alisema hali hiyo ya mvua kubwa  pia itayakumba maeneo ya Kaskazini (Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba) kuanzia mwishoni mwa mwezi huu.
Alisema mikoa ya Kigoma, Tabora na Rukwa pamoja na Kanda ya Juu Kusini na katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Mbeya pia itakuwa na mvua nyingi kuanzia Novemba Mosi.
Hata hivyo, alisema katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Morogoro mvua zitakuwa za kawaida  kuanzia mwishoni mwa mwezi huu.
Alisema pia mvua zinatarajiwa kuwa za kawaida katika mikoa ya Dodoma na Singida, huku mikoa ya Lindi na Mtwara ikitarajiwa kuwa na mvua za wastani mpaka juu ya wastani kuanzia mwanzoni mwa Novemba.
Dk Kijazi aliongeza kusema kutokana na hali hiyo ya mvua maeneo mengi ya nchi yatakuwa na unyevunyevu mkubwa hali ambayo inaweza kupelekea mazao kuhalibika na kuzitaka mamlaka husika na wananchi kuchukua tahadhari na kuendelea kufuatilia kwa karibu taarifa zitakazotolewa na mamlaka hiyo.
 Awali, kulikuwa na wasiwasi wa kutokea kwa mvua za El Nino kutokana na kuongezeka kwa joto hadi kufikia nyuzi 2.5 katika Bahari ya Pacific na mwitikio wake kuonekana kwenye Bahari ya Hindi maeneo ya Pwani ya Afrika Mashariki.
Hata hivyo jana, Dk Kijazi, alisema kuwa pamoja na kuwa joto limeongezeka katika Bahari ya Pacific, bado joto la Bahari ya Hindi halijawa kubwa sana kama ilivyokuwa mwaka 1997 kulipotokea El-nino nchini.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!